Marekani iache kuleta siasa kwenye COVID
2 Agosti 2021Baadhi ya mataifa yameanza kuripoti kupungua kwa maambukizi mapya virusi vya corona ikilinganishwa na ripoti za wiki mbili kabla. Lakini hata hivyo takwimu za kidunia zinaonyesha kwamba janga hili la COVID-19, wala halitamalizika hivi karibuni. Na huko nchini Israel, mamlaka zimeanza kutoa dozi ya tatu ya chanjo kwa wazee, huku baadhi ya makampuni yakipandisha bei ya chanjo hizo.
Takwimu zinaonyesha kwamba hali imeimarika kiasi. Mataifa 116 yameripoti ongezeko la visa vya maambukizi katika kipindi cha wiki mbili zilizopita, ikilinganishwa na siku 14 kabla. Mataifa mengi ya Asia, Amerika, Afrika na Ulaya yameripoti ongezeko la mara mbili ikilingaishwa na wiki mbili zilizopita, huku maeneo kama ya Vatican, Visiwa vya Marshall, Samoa, Visiwa vya Solomon na Vanuatu yakiwa hayana ripoti ya kisa hata kimoja cha maambukizi.
Soma Zaidi:Polisi wa Ufaransa wamekabiliana na waandamanaji wanaopinga pasi ya afya
Hadi sasa watu milioni 4.4 wamekufa baada ya kuambukizwa virusi vya corona kote ulimweguni.
Marekani yaibua tea madai ya chimbuko la virusi kuwa ni Wuhan.
Huko Washington, ripoti ya wabunge wa chama cha Republican iliyochapishwa hii leo imesema kuna ushahidi wa kutosha kwamba virusi vya corona vilitokea kwenye kituo cha utafiti cha nchini China, ikiwa ni hitimisho ya kile ambacho taasisi za kijasusi za Marekani bado hawajaafikiana.
Mbunge mwandamizi wa Republican katika kamati ya mahusiano ya kigeni Mike McCaul pia ametaja ushahidi wa kutosha kuwa wanasayansi wa taasisi yaWuhan ya utafiti wa virusi, wakisaidiwa na wataalamu wa Marekani kwa ufadhili wa China na Marekani walikuwa wanatengeza virusi hivyo kuathiri wanadamu na udanganyifu kama huo huenda ukafichwa.
Wametaka uchunguzi utakaohusisha vyama vyote viwili kuhusiana na chimbuko la virusi hivyo.
Na huku hayo yakiendelea, wanadiplomasia nchini Misri wameiomba Marekani na mataifa mengine kuancha kuingiza siasa kwenye janga hilo na badala yake kushirikiana ili kupunguza kusambaa zaidi kwa maambukizi. Mkurugenzi wa baraza la mahusiano ya nje na waziri wa zamani wa mambo ya kigeni wa Misri Ezzat Saad amesema Marekani inatakiwa kuacha kabisa kuchanganya vipaumbele wakati ulimwengu ukipambana na COVID-19 kisayansi.
Amesema, "Kuingiza siasa kwenye virusi, chimbuko lake na hata siasa za chanjo, ni kuchanganya vipaumbele, na kuzuia mchakato wa mshikamano wa kimataifa na ushirikiano katika kupambana na janga hilo. Kuanzia mwanzo, China ilijua majukumu yake ikilinganishwa na msimamo mwingine, ambao ni wa Marekani, ambao hutafuta masilahi ya kibinafsi bila kujali maslahi ya jamii nzima ya kimataifa. "
Ujerumani yataka kuanza kampeni za chanjo kwa watoto wa kuanzia miaka 12.
Hapa Ujerumani mamlaka zinajipanga kuanza kuhamasisha utoaji wa chanjo kwa watoto wa kati ya miaka 12 hadi 17, wakati wasiwasi ukiongezeka wa kusambaa kwa kirusi kibaya kabisa kinachojibadilisha cha Delta.
Waziri wa afya wa Ujerumani Jens Spahn na mawaziri wa afya wa majimbo yote 16 wanatarajiwa kukubaliana mapendekezo yaliyoandaliwa na wizara hiyo hii leo licha ya kutokuwepo kwa ruhusa rasmi ya mchakato huo kutoka kwa msimamizi wa kitaifa wa chanjo, STIKO.
Taasisi ya madawa ya Ulaya, EMA imeidhinisha matumizi ya BioNTech-Pfizer and Moderna kwa watoto kuanzia miaka 12.
Na huko Israel, mamlaka zimeanza kutoa dozi ya tatu ya chanjo kwa wazee wa zaidi ya miaka 60 ili kukabiliana na kirusi cha Delta na kuimarisha uwezo wa miili wa kujilinda na maambukizi.
Mashirika: DW/RTRE