Marekani : Sudan Kusini yashindwa kutekeleza amani
1 Aprili 2022Marekani imesema uongozi wa Sudan Kusini unashindwa kutekeleza baadhi ya vipengele vya makubaliano ya amani yaliyosainiwa mwaka 2018, na kuonya kuwa itaendelea kuwawekea vikwazo wanaochochea mzozo.
Wizara ya mambo ya nje katika ripoti yake kwa bunge la Congress, ambayo haijatangazwa hadharani, imesema serikali ya umoja wa kitaifa ilikuwa inasuasua katika kutekeleza ahadi muhimu zilizotolewa chini ya makubaliano hayo, na walishindwa kutekeleza masuala muhimu katika wakati.
Ripoti hiyo imesema miaka 10 baada ya uhuru, Sudan Kusini inasalia kuwa taifa dhaifu sana na linalokabiliwa na utawala dhaifu, usalama tete na usimamizi mbaya wa fedha na ufisadi mkubwa.
Taifa hilo lilipata uhuru kutoka Sudan mwaka 2011 lakini lilitumbukia katika mapigano miaka miwili baadaye, baada ya vikosi tiifu kwa Salva Kiir na kiongozi wa zamani wa waasi, ambaye kwa sasa ni makamu wa kwanza wa rais, Riek Machar, kupigana katika mji mkuu.