Marekani yahimiza marufuku ya silaha dhidi ya Sudan Kusini
26 Aprili 2017Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Nikki Haley aliliambia baraza hilo kwamba matakwa ya Umoja wa Mataifa kuhusu usitishaji mapigano, kuruhusiwa kwa wafanyakazi wa misaada na kurejewa kwa mazungumzo ya kisiasa yalikuwa yamepuuzwa kabisa na serikali ya Rais Salva Kiir, na kulitolea mwito baraza hilo kusonga mbele na zana lilizonazo, kama vile vikwazo zaidi na marufuku ya silaha, vinginevyo vurugu na unyama vitaendelea.
Haley alisema lazima waiambie serikali ya Sudan Kusini kwamba hawawezi kuvumilia tena hali inayoendelea nchini Sudan Kusini. Ufaransa na Uingereza zimeunga mkono wito huo wa Marekani wa kuchukuliwa hatua kali zaidi, lakini Urusi ilisema hakukuwa na haja ya kuweka marufuku ya silaha, na China ililihimiza baraza hilo kuwa na mtazamo chanya zaidi katika kulishughulikia suala la Sudan Kusini.
Msukumo mpya wa marufuku ya silaha
Matamshi ya Balozi Haley yaliashiria kwamba utawala mpya wa Marekani utajaribu tena kushinikiza mwisho wa mauzo ya silaha na vikwazo kwa wale wanaodhoofisha juhudi za amani. Alisema iwapo wanataka kuona njaa ikiendelea Sudan Kusini, basi waendelee kutofanya chochote, na kuongeza kuwa kuwasadia watu wa Sudan Kusini hakuhusu matumaini wala matakwa, lakini kunahusiana na hatua, na kulitaka baraza hilo kuchukuwa hatua.
"Ukame nchini Sudan Kusini umesababishwa na binadamu. Ni matokeo ya mgogoro unaoendelea nchini humo. Ni matokeo ya kampeni ya wazi dhidi ya raia. Ni matokeo ya kuwazuwia watu wenye njaa kupata chakula na dawa ambavyo vitasaidia kuokoa maisha yao. Hiyo ndiyo sababu kuna ukame nchini Sudan Kusini," alisema Balozi Haley.
Haley alisema Kiir na serikali yake walikuwa wananufaika na migawanyiko ndani ya baraza la usalama. Baraza hilo lenye wanachama 15 lilishindwa mwezi Desemba kupata kura 9 ili kupitisha azimio la kuiwekea Sudan Kusini marufuku ya kuuziwa silaha na vikwazo zaidi, licha ya onyo kutoka kwa maafisa wa Umoja wa Mataifa kuhusiana na uwezekano wa kutokea mauaji ya halaiki. Nchi nane wanachama zikiwemo Urusi na China zilijizuwia kupiga kura.
Mjumbe aeleza hali inatisha
Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa David Shearer aliliambia baraza kuwa hali inatisha, kukiwa na mapigano Wau, mji wa pili kwa ukubwa nchini Sudan Kusini, na katika majimbo ya Equatoria Magharibi, Equatoria ya Kati na Equatoria ya Mashariki. Shearer alisema kimsingi hakuna sehemu ilio salama kutokana na mapigano nchini Sudan Kusini, huku kukiwa hakuna juhudi zozote za pamoja kwa upande wowote kuheshimu mpango wa usitishaji mapigano.
Mwezi Februari Sudan Kusini na Umoja wa Mataifa zilitangaza rasmi ukame katika baadhi ya maeneo ya jimbo la Unity, unaowaathiri watu 100,000, mgogoro ambao Umoja wa Mataifa ulisema ulisababishwa na binadamu na ungezuilika. Kamati ya Umoja wa Mataifa mwezi uliopita ilipendekeza marufuku ya uuzwaji wa silaha, katika ripoti iliyosema serikali ilikuwa inatumia mapato ya mafuta kwenye ununuzi wa sialha wakati raia wake wakiteseka.
China, ambayo imetuma walinda amani Sudan Kusini, na Urusi zimseisitiza kuwa mataifa ya kanda yashirikishwe zaidi katika kuutafutia ufumbuzi mgogoro huo.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe,rtre,ape
Mhariri: Josephat Charo