Marekani yaidhinisha chanjo ya tatu ya Covid-19
28 Februari 2021Mamlaka ya udhibiti wa chakula na dawa ya Marekani FDA, imesema kuwa chanjo ya kampuni hiyo inayotolewa kwa dozi moja ina ufanisi mkubwa katika kuzuia Covid-19 pamoja na aina mpya ya virusi cha corona.
Chanjo hiyo ni ya tatu kuidhinishwa kutumika nchini Marekani baada ya chanjo za Pfizer na Moderna kuidhinishwa mwezi Desemba mwaka uliopita.
Ithibati kutoka FDA inafuatia maoni yaliyotolewa na jopo la wataalamu huru waliosema chanjo hiyo imekidhi vigezo vya matibabu.
Mamlaka ya FDA imethibitisha kuwa chanjo ya Johnson&Johnson itatolewa kwa watu wenye umri wa kuanzia miaka 18 na zaidi.
Kuidhinishwa kwake kunaongeza nguvu kwenye kampeni ya taifa ya utoaji chanjo nchini Marekani ambayo ilisuasua kwa wiki kadhaa.
Karibu raia milioni 47.2 wa Marekani tayari wamepatiwa dozi ya kwanza ya chanjo ya corona, kulingana na taasisi ya kupambana na magonjwa nchini humo.
Chanjo zitakuwa tayari mwezi unaokuja
Kampuni inayozalisha chanjo hiyo ya Johnson &Johnson yenye makao yake mjini New Jersey imesema dozi milioni 20 zitakuwa tayari kusambazwa nchini Marekani mwishoni mwa mwezi Machi.
Kampuni hiyo inalenga kuipatia Marekani dozi milioni 100 za chanjo hiyo kabla ya mwezi Juni.
Jambo la faraja ni kwamba chanjo ya Johnson & Johnson inaweza kuwahifadhiwa kwenye baridi la wastani mfano wa jokofu la nyumbani tofauti na chanjo nyingine hususani ile ya kampuni ya Moderna na Pfizer zinazohitaji kutuzwa kwa kiwango cha juu cha baridi.
Suala lingine la kutia moyo ni kwamba utafiti wa mabaara umeonesha chanjo ya Johnson & Johnson imeonesha kuwa na uwezo wa asilimia 66 kutoa kinga dhidi ya aina mpya ya virusi vya corona. Kadhalika ina uwezo wa asilimia 85 ya kuzuia maambukizi makali ya virusi hivyo.
Rais Biden asifu mafanikio hayo
Rais wa Marekani Joe Biden amesema hayo ni maendeleo ya kutia moyo katika juhudi za kumaliza janga hilo.
"Tunafahamu kwamba watu wengi zaidi wanapochanjwa, ndiyo kwa haraka tutaweza kuvishinda virusi hivi, kujumuika tena na marafiki na wapendwa wetu na kufungua tena shughuli za uchumi" amesema Biden katika taarifa aliyoitoa kufuatia ithibati iliyotolewa na FDA.
Wakati huohuo Afrika Kusini jana ilipokea shehena ya pili ya chanjo ya Johnson & Johnson kwa ajili ya COVID-19, itakayosaidia katika mapambano ya janga hilo.
Taifa hilo linatumai chanjo hiyo itasaidia kwa sehemu kubwa kupambana na aina mpya ya virusi vya corona vilivyozuka nchini na ambavyo chanjo zilizotangulia zimeonesha uwezo mdogo wa kukabiliana nayo.