1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yaitaka Korea kurejea katika meza ya mazungumzo

Thelma Mwadzaya20 Februari 2009

Waziri wa mambo ya kigeni wa Mareakni, Hillary Rodham Clinton, ameitaka Korea Kaskazini irejee kwenye mazungumzo kuhusu mpango wake wa nyuklia.

https://p.dw.com/p/Gy5O
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Hillary Clinton akiwa ziarani KoreaPicha: picture alliance / abaca

Ameyasema hao kwenye mkutano na waandishi wa habari mjini Seoul nchini Korea Kusini.


Akiwa katika kituo chake cha tatu cha ziara yake ya nchi nne barani Asia, Bi Hillary Clinton ameipongeza Korea Kusini kwa kuendeleza demokrasia na maendeleo lakini akaikosoa vikali Korea Kaskazini.

"Ufanisi wa kidemokrasia na kimaendeleo wa Jamhuri ya Korea unadhihirisha tofauti kubwa ya ukatili na umaskini uliopo upande wa pili wa mpaka wa Korea Kaskazini. Nawapongeza watu wa Korea Kusini na viongozi wenu kwa uvumilivu na ari yenu licha ya matamshi na vitendo vya uchokozi vya Korea Kaskazini ."


Waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani, Hillary Clinton, pamoja na mwenzake wa Korea Kusini, Yu Myung Hwan, wamesema baada mkutano wao mjini Seoul, kwamba nchi zao hazitokubali Korea Kaskazini yenye silaha za nyuklia. Bi Clinton amevieleza vita vya maneno vya Korea Kaskazini kuwa uchokozi usiofaa na kuihimiza nchi hiyo ifanye mazungumzo na Korea Kusini. Ameionya Korea Kaskazini iache matamshi ya uchokozi kama inataka kuboresha uhusiano wake na Marekani.


"Korea Kaskazini haitapata uhusiano tofauti na Marekani huku ikiitukana na kukakataa kufanya mazungumzo na Jamhuri ya Korea. Tunaitaka serikali ya Korea Kaskazini ikomeshe vita vya maneno ya uchokozi na visivyofaa."


Waziri Clinton na mwenzake, Yu, wametaka mazungumzo ya pande sita yanayolenga kuumaliza mpango wa nyuklia wa Korea Kaskazini yaanze tena. Waziri Clinton pia amesema watajadiliana kuhusu njia muafaka za kukabiliana na Korea Kaskazini ili kuwasilisha msimamo wa pamoja juu ya maswala yote ya kutia wasiwasi. Amesema kwa sasa jambo linalotakiwa kushughulikiwa haraka ni kuharibu vinu vyote vya nyuklia na kupata thibitisho na makubaliano ya kuumaliza mpango wa nyuklia wa Korea Kaskazini.


Kwenye mkutano wa mjini Seoul waziri Hillary Clinton ametangaza kuteuliwa kwa Stephen Bosworth kuwa mpatanishi mpya mkuu wa Marekani katika mzozo wa Korea Kaskazini. Bosworth aliyekuwa zamani balozi wa Marekani nchini Korea Kusini, atashughulikia ukiukaji wa haki za binadamu na maswala ya kibinadamu ya Korea Kaskazini. Atashirikiana na Korea Kusini, Japan, China na nchi nyingine kutafuta njia za kuishawishi Korea Kaskazini irudi kwenye meza ya mazungumzo kujaribu kutanzua mzozo wa nyuklia.


Bi Clinton amejadiliana na waziri Yu kuhusu maswala ya biashara na kuipongeza Korea Kusini kwa juhudi zake nchini Afghanistan.


"Tumezungumzia pia njia za kufanya kazi pamoja kupanua biashara ili izinufaishe nchi zote mbili. Naishukuru Korea Kusini kwa kujitolea kusaidia kazi yetu nchini Afghanistan, kuzilinda bahari zetu kutokana na uharamia na kuahidi kushirikiana nasi kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa duniani."


Marekani na Korea Kusini zimekubaliana kuuimarisha muungano wao wa kijeshi. Marekani ina wanajeshi 28,500 nchini Korea Kusini ambao wamewekwa nchini humo ili kuzuia kitisho cha Korea Kaskazini.