Marekani yapeleka wanajeshi Gabon ikihofia machafuko Congo
5 Januari 2019Katika barua aliyowasilisha Bungeni, Trump alisema wanajeshi Zaidi huenda wakapelekwa katika eneo hilo kutokana na uwezekano wa kuzuka maandamano yenye ghasia.
Barua ya Trump imesema wanajeshi hao "watabaki katika eneo hilo hadi hali ya usalama katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo utakapokuwa imara na uwepo wao usihitajike tena.”
Siku ya Alhamisi Wizara ya Mambo ya Nchi za Kigeni ya Marekani ilitoa wito kwa Tume ya Uchaguzi – CENI kuhakikisha kuwa kura zinahesabiwa kwa umakini na kutishia kuwawekea vikwazo watakaohujumu mchakato huo au kutishia Amani na utulivu wa nchi hiyo.
Ulaya na Afrika zaongeza mbinyo
Umoja wa Ulaya na Umoja wa Afrika ziliiongezea mbinyo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, zikiitaka iheshimu matakwa ya wapiga kura wakati muda wa mwisho wa kutoa matokeo ukikaribia.
Kuna ongezeko la matarajio kuwa wasimamizi wa uchaguzi watachelewesha matokeo ya mwanzo yanayotarajiwa Jumapili – hatua inayoweza kuongeza hofu katika nchi hiyo isiyokuwa na utulivu.
"Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo iko katika wakati wa kihistoria kuelekea mpito wa kidemokrasia,” umesema Umoja wa Ulaya. Umetoa wito kwa maafisa kuhakikisha matokeo yananayosubiriwa yatatimiza matakwa ya wapiga kura. Ombi sawa na hilo limetolewa na Umoja wa Afrika – AU baada ya kupewa tathmini kutoka kwa mkuu wa timu ya uangalizi wa uchaguzi yenye wanachama 80.
"Ni muhimu kuheshimu matokeo ya uchaguzi,” amesema mkuu wa AU Faki Mahamat kwenye Twitter.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilikutana katika kikao cha faragha kuujadili uchaguzi huo, lakini baada ya masaa mawili ya mkutano likashindwa kukubaliana kuhusu taarifa kwa vyombo vya habari. Wanadiplomasia wamesema nchi kadhaa yakiwemo mataifa ya Kiafrika yalisema hatua ya aina hiyo itakuwa ya mapema mno.
Wapinzani wahofia wizi wa kura
Upinzani nchini humo unahofia kuwa matokeo hayo huenda yakafanyiwa uchakachuaji ili kumpa ushindi mtu ambaye Rais Joseph Kabila anapendelea awe mrithi wake, waziri wake wa zamani wa mambo ya ndani Emmanuel Ramazani Shadary. Anakabiliwa na wapinzani wawili wakubwa – Martin Fayulu, mkurugenzi wa zamani wa kampuni ya mafuta aliyejitosa saisani, na Felix Tsisekedi, mkuu wa UDPS, chama kikongwe kabisa na kikubwa cha upinzani nchini humo.
CENI imesema inakabiliwa na matatizo ya kimiundo na usafiri katika mchakato wa kukusanya makatarasi ya kura kutokana na ukubwa wa nchi. Iliiashiria kuwa huenda ikaahirisha matokeo ya mwanzo – yanayotarajiwa Jumapili, kabla ya kutangazwa matokeo kamili Januari 15 na rais mpya kuapishwa siku tatu baadaye.
Kanisa Katoliki katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ambalo lilikuwa na maelfu ya waangalizi wa uchaguzi limetangaza kuwa linafahamu nani aliyeshinda uchaguzi huo kutokana na matokeo yao ya kura hizo. Limeitaka CENI "kuchapisha matokeo kwa kuzingatia ukweli na sheria.”
Wasiwasi wa kimataifa pia umechochewa na hatua ya serikali kukata huduma za intaneti, kuifungia redio ya shirika la utangazaji la Kifaransa Radio Frane International na kumfukuza nchini humo mwanahabari wake. "Juhudi hizi za kuwanyamazisha wapinzani huenda zikagonga mwamba na kusababisha madhara makubwa wakati matokeo yatakapotangazwa,” Ofisi ya Haki za Binaadamu ya Umoja wa Mataifa imeonya.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri: Jacob Safari