Marekani yawaonya viongozi wa Sudan Kusini
21 Julai 2017Naibu Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Michele Sison, amesema mazungumzo hayo yaliyoandaliwa na Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika (IGAD) ni "nafasi ya mwisho" ya kuyaokoa makubaliano ya amani ya Agosti 2015.
Sison amesema ikiwa viongozi hao watashiriki katika mazungumzo hayo na kuheshimu muda wa mwisho uliowekwa, Marekani itapitia upya msimamo wake na vipaumbele katika msaada kwa ajili ya makubaliano ya amani na utekelezaji wake.
Kulikuwa na matumaini makubwa kwamba taifa hilo changa lingejipatia amani baada ya kujipatia uhuru wake kutoka kwa taifa jirani la Sudan mwaka 2011, lakini limetumbukia katika machafuko ya kikabila tangu Desemba 2013 baada ya vikosi vitiifu kwa Rais Salva Kiir kutoka kabila la Dinka kuanzisha mapigano na vile vinavyomfuata Riek Machar, aliyekuwa makamu wake wa rais ambaye ni Mnuer.
Makubaliano ya amani ya 2015 hayajazuia mapigano na msaidizi wa katibu mkuu katika ulinzi wa amani El Ghassim Wane, ameliambia baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hapo jana Alhamis kuwa mazingira ya usalama bado yamesalia tete na kwamba Sudan Kusini inahitaji usitishaji mapigano wa ufanisi na wa kuaminika.
"Mchakato wa amani Sudan Kusini unaendelea kukabiliwa na changamoto ambazo zinatakiwa kuwa kipaumbele ikiwa tunatumia fursa zilizojitokeza kwa kuwaleta askari wa RPF mjini Juba na kuirejesha nchi katika mstari wa amani na usalama wa kudumu," amesema Wane.
Mgogoro wa Sudan Kusini umewaua makumi kwa maelfu ya watu na kuwalazimisha wengine milioni 3.5 kuyakimbia makazi yao.
Ili kuzishinikiza pande zote kuchukua hatua, Sison ameliomba Baraza la Usalama kuweka vikwazo kwa watu ambao wanakwamisha amani na vikwazo vya silaha.
Rais wa zamani wa Botswana Festus Mogae ambaye ni mwenyekiti wa kamati inayofuatilia na kutathmini juhudi za amani Suda Kusini, ameliambia Baraza la Usalama kwamba amewashirikisha viongozi wa kitaifa na kikanda akiwemo Machar mwenyewe ambaye kwa hivi sasa anaishi Afrika Kusini. " Naamini kuwa mbinu thabiti za IGAD, Umoja wa Afrika, Umoja wa Mataifa, Jumuiya za Kimataifa na ushirikiano wa viongozi wa Sudan Kusini tunaweza kurejesha msingi uliopotea na kurejesha matamaini ya watu wa Sudan Kusini," amesema Festus Mogae.
Naye kiongozi wa upinzani anayeishi uhamishoni Riek Machar amekataa kukemea machafuko au kutangaza usitishaji mapigano wa pamoja na badala yake ameomba mazungumo mapya ya amani nje ya taifa hilo.
Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AP/Reuters
Mhariri: Mohammed Khelef