1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Martin Kobler aikemea serikali ya Congo

Mjahida28 Oktoba 2014

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, amekemea hadharani hatua ya serikali ya nchi hiyo kumfukuza mkuu wa ofisi ya haki za binaafamu wa Umoja huo nchini Congo Scott Campbell.

https://p.dw.com/p/1Dd7U
Mjumbe wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Martin Kobler
Mjumbe wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Martin KoblerPicha: Dirke Köpp

Scott Campbell, alifukuzwa nchini humo baada ya ripoti ya Umoja huo kuishutumu polisi kwamba iliwanyanyasa raia katika oparesheni ya kuwakamata wahalifu mjini Kinshasa.

"Ni wale wanaokiuka haki za binaadamu wanaokwepa adhabu ndio wanaoharibu sura ya Congo na kudhoofisha taasisi za usalama, sio wale wanaoweka wazi mambo haya," alisema muakilishi wa Umoja wa Mataifa nchini Congo Martin Kobler wakati alipokuwa akilihutubia Baraza la Usalama la Umoja huo lililo na nchi wanachama 15.

Aidha Martin Kobler ameongeza kwamba tayari ameiomba serikali kufikiria uamuzi wake huku akisema ana imani kubwa kabisa kwa namna Scott Campbell anavyofanya kazi yake kwa utaalamu ya hali ya juu pamoja na muda wake katika kazi yake na kwamba anasimama naye imara katika ripoti iliotolewa na kuchukua jukumu kamili.

Wanajeshi wa kulinda amani Congo
Wanajeshi wa kulinda amani CongoPicha: DW/D. Köpp

Licha ya hayo mjumbe wa Congo katika Umoja wa Mataifa Ignace Gata Mavita wa Lufuta, alichukua hatua ya kumfukuza kazi Campbell, mara moja huku akiliambia baraza la usalama la Umoja huo, kwamba tabia yake ya kuchukiza ya namna anavyoripoti mambo, imeonyesha kuwa amekataa kutilia maanani maoni na ufafanuzi uliotolewa kwake na mamlaka za serikali husika.

Balozi wa Rwanda alalama juu ya jeshi la MONUSCO

Wakati huo huo balozi wa Rwanda katika Umoja huo Eugene Richard Gasana ameelezea kutoridhishwa na ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Congo, unaojulikana kama MONUSCO, kutochukua hatua yoyote dhidi ya waasi wa Rwanda Mashariki mwa Congo ambao ni miongoni mwa wale waliohusika na mauaji ya halaiki ya mwaka 1994 katika nchi jirani ya Rwanda.

Waasi hao wa Rwanda wanaojulikana kama FDLR wamekuwa wakipuuza muda wa miezi sita waliowekewa na viongozi wa Afrika wa eneo la maziwa makuu kusalimisha silaha zao. Hatua hii imeongeza shinikizo kwa Monusco kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya kundi hilo la waasi.

Waasi wa FDLR
Waasi wa FDLRPicha: DW/S. Schlindwein

Utakumbuka kuwa wataalamu wa Umoja wa Mataifa waliishutumu Rwanda kuwaunga mkono waasi walioshindwa wa M23 madai ambayo Rwanda hadi sasa inakanusha vikali. Lakini serikali nyengine za Magharibi zinazounga mkono ripoti ya wataalamu hao zilisimamisha kwa muda msaada wao kwa Rwanda.

Hata hivyo Martin Kobler amesema bado kumebakia miezi miwili na siku tano kabla ya muda wa waasi kusalimisha silaha zao kumalizika. Kobler amesema iwapo hilo halitafanyika MONUSCO itachukua hatua.

Mwandishi: Amina Abubakar/Reuters

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman