Mashaka yaugubika muafaka wa DRC
2 Januari 2017Ijapokuwa matumaini yaliyopo baada ya kutiwa saini mkataba huo wa kisiasa, lakini wengi wanaamini kwamba njia ya kuelekea kwenye uchaguzi mkuu bado ina mikunjo mingi. Kwa hiyo ni lazima kila upande ubebe dhamana yake kwa kufanikisha taratibu ya uchaguzi.
Vital Kamerhe, mmoja wa viongozi wa upinzani waliotia saini mkataba huo, aliiambia DW kwamba ni lazima kuanzia sasa kila mtu awajibike.
"Tutakuwa na majadiliano ya kipekee wiki hii. Kulikuwa na kalenda ya wazi itakayoipa kila upande majukumu na dhamana yake, kwa ajili ya utekelezwaji wa mkataba huu."
Chama tawala kilitangaza kwamba kimetia saini ya mkataba huo kwa mashaka, kwa sababu kuna vyama vingine vya upinzani ambavyo vimesusia kutia saini. Waziri wa Mambo ya Ndani Ramadhani Shadari, ambaye pia ni naibu katibu mkuu wa chama tawala, alisema kwamba makubaliano ya kuweko na uchaguzi ifikapo mwishoni mwa mwaka huu ni jambo la kukisia tu.
"Tarehe iliyotolewa na ambayo tunakubaliana ni makadirio pekee. Naomba tusiwadanganye raia wetu kwa sababu maandalizi ya uchaguzi siyo maswala ya kisiasa, bali ya kiufundi. Na ikiwa haitowezekana kuweko na uchaguzi kwenye tarehe hiyo, basi kutakuweko na tathimi kwa undani, na ndio sababu tumeunda kamati ya kitaifa ya ufuatiliaji wa mkataba huo."
Wataalamu wa maswala ya uchaguzi wanasema kwamba kuandaa kwa pamoja uchaguzi wa rais, wa bunge la kitaifa na majimbo ni changamoto kubwa kwa serikali na tume huru ya uchaguzi. Wataalamu hao wanapendekeza kuweko na uhalisia wakati wa kutangazwa kwa kalenda ya uchaguzi na tume ya uchaguzi.
Vyama kadhaa vya upinzani vilisusia pia kutia saini mkataba huu wa hivi sasa, kama vile chama cha MLC. Waziri Mkuu Samy Badibanga na baadhi ya vyama vilivyoshiriki kwenye mazungumzo ya Oktoba pia wamesusia kutia saini mkataba huu.
Kwenye hotuba yake mbele ya wajumbe wa upinzani na chama tawala, Askofu Marcel Utembi, kiongozi wa kongamano la maaskofu wa Kongo ambaye alisimamia mazungumzo hayo ya kisiasa alihimiza pande zote kuyapa kipaumbele maslahi ya kitaifa.
"Kuweko na mkataba wa kisiasa ni jambo moja, na kuutekeleza ni jambo jingine, kwa hiyo Kanisa Katoliki linatowa mwito kwa kila mmoja wetu aonyeshe uzalendo kwa maslahi ya taifa letu", alisema Aslofu Utembi.
Miongoni mwa yaliyoafikiwa ni pamoja na Rais Joseph Kabila kusalia madarakani hadi atakapochaguliwa rais mpya na wadhifa wa waziri mkuu kupewa upinzani wa Rassemblement na pia kuundwa kamati ya kitaifa ya ufuatiliaji wa mkataba.
Mwandishi: Saleh Mwanamilongo/DW Kinshasa
Mhariri: Iddi Ssessanga