1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

G-20 yapitisha mkakati dhidi ya IS

17 Novemba 2015

Mashambulio ya kigaidi ya Paris na athari zake ndio mada kuu magazetini pamoja na kuzingatia mpango uliopitishwa na viongozi wa G-20 mjini Antalya nchini Uturuki

https://p.dw.com/p/1H71I
Rais wa Ufaransa Francois Hollande akihutubia wawakilishi wa bunge na Senet katika kasri la VersaillesPicha: Reuters/Philippe Wojazer

Tuanzie na gazeti la "Stuttgarter Nachrichten linalotilia mkazo maneno yafuatiwe na vitendo.Gazeti linaendelea kuandika: "Angalao tangu yalipotokea mashambulio ya kigaidi mwishoni mwa wiki iliyopita imedhihirika kwamba nchi za magharibi zimechangia kwa sehemu kuibuka zimwi hili katili linaloeneza mashambulio yake katika takriban sehemu kubwa ya dunia.Kuliteketeza panahitajika zaidi ya maneno matupu.Anaetaka kumshinda nguvu zimwi la dola la kiislam-IS anabidi kwanza kile anachokisema kiaminike.

Gazeti la "Der neue Tag" linachambua uamuzi wa Ufaransa wa kulipiza kisasi na kuandika:"Hata kama jibu la Ufaransa la kuhujumu kwa mabomu vituo vya IS linaeleweka,hata hivyo juhudi za nchi za magharibi kuuvunja nguvu ugaidi nchini Afghanistan,au Iraq kwa kutuma vikosi vya nchi kavu ,kufanya mashambulio ya angani na kutumia ndege zisizokuwa na rubani sio tu zimeshindwa vibaya,zimeufanya ulimwengu uzidi kuwa hatari.Demokrasia ya kinga inaanzia nyumbani kwa kuyapatia jibu kali na la haraka masuala ya kuwapokonya uraia (wenye uraia wa nchi mbili) au kuwafukuza na kuwapiga marufuku ya kuingia nchini wafuasi wa itikadi kali na wale wenye kutoa hutuba za kueneza chuki.

Mpango wa G-20 kupambana na magaidi

Mashambulio ya kigaidi ya Paris yamegubika pia mkutano wa viongozi wa mataifa 20 yanayoendelea na yale yaliyoendelea-G-20 mjini Antalya nchini Uturuki.Gazeti la "Freie Presse" linaandika:"Viongozi wa mataifa na serikali wa G-20 wamekubaliana kwa dhati kuhusu mpango madhubuti wa kupambana na ugaidi.Kwa mfano wanapanga kuwafungia njia za kujipatia fedha magaidi wa kimataifa.Sasa kwanini hawajafanya hivyo tangu zamani?Hapo bila ya shaka na kama kawaida kulikuwa na masilahi tofauti,hali ya kutojua la kufanya na pia unafiki.Kuuvunja nguvu ugaidi ni mtihani mgumu unaohitaji muda mrefu na ambao nguvu za kijeshi pekee hazitoshi kuupatia ufumbuzi.Lakini wanamgambo wa kigaidi wanajipatia nguvu tu kule ambako utawala hauna nguvu.Syria mpya inaweza kuwavunja nguvu IS kule kule waliko.Na jee hilo linawezekana?Kwa vyovyote vile língekuwa hatua muhimu hata kama ni ndogo,bora kuliko hiyo hakuna.

Wakimbizi wasitengwe

Na hatimae gazeti la "Rhein-Necker-Zeitung"linatahadharisha dhidi ya kuwaachilia mbali wakimbizi kutokana na mashambulio ya kigaidi ya Paris.Gazeti linaendelea kuandika:" Kama kuna tulichojifunza kutokana na mashambulio ya kigaidi ya Paris basi ni hili;tunabidi tuwakumbatie wakimbizi wetu."Tuwakumbatie katika jamii.Tunabidi tuwapatie nafasi ya kuchangia katika maisha ya kila siku humu nchini.Hawastahiki kuishi peke yao katika maeneo ya madongo poromoka-wanabidi waishi pamoja na jamii.Watoto wanabidi wapelekwe shule,watuwazima wapatiwe kazi walizosomea.Kwasababu hapo tu ndipo tutakapoweza kuepusha balaa la kuchipuka jamii mbili zinazoishi kila moja upande wake.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri:Josephat Charo