Mashitaka ya Malema wa ANC kuendelea kusikilizwa
2 Septemba 2011Chama hicho kilianza kusikiliza mashitaka ya kinidhamu dhidi ya Malema mapema wiki hii, ambaye pamoja na mambo mengine anatuhumiwa kusababisha mifarakano katika uongozi wa chama hicho.
Kutokana na uamuzi uliofikiwa leo, ina maanisha kwamba mashitaka dhidi ya kiongozi huyo wa vijana yataendelea kusikilizwa, na endapo atapatikana na hatia basi inawezekana akasimamishwa katika chama hicho.
Shirika la Habari la Uingereza, Reuters, limenukuu maneno machache kutoka katika taarifa iliyotolewa na kamati ya nidhamu ya ANC yanayosema" Kamati ya Taifa ya Nidhamu ya ANC imelitupilia mbali ombi la Comrade Julius Malema la kutaka aondolewe mashitaka yake"
Kauli hiyo ya kamati imetolewa baada ya kutathimini hoja 22 zilizowasilishwa na Malema. Nje ya makao makuu ya ofisi ya ANC mjini Johannesburg kulikuwa na idadi kubwa ya polisi, baada ya jumanne polisi hao kuwasambaratisha wafuasi wa Malema na kusababisha waandishi wa habari wanne kujeruhiwa.
Mashitaka hayo yanaonekana kama mgongano wa kimaslahi kati ya Zuma na Malema ambae anaungwa mkono na idadi kubwa ya watu weusi nchini humo kufuatia wito wake wa kutaka nchi hiyo inyang'anye migodi na mashamba makubwa ya wazungu ili yarejeshwe katika mkono wa umma na kunufaisha raia wote.
Malema, mwenye umri wa miaka 30, anaweza kuwa kiongozi wa baadae wa ANC ikiwa ataondolewa mashitaka yake, ambapo mustakabli wa Zuma utakuwa mashakani.
Zuma anakabiliwa na changamoto ya mkutano mkubwa wa ANC mwishoni mwa 2012, pale ambapo chama hicho kitapiga kura ya kumchagua kiongozi wake.
Wachambuzi wanasema atakuwa katika nafasi nzuri ya kurejea tena katika nafasi yake pale ambapo Malema hatokuwepo madarakani, lakini mambo yatakuwa tofauti pale ambapo kijana huyo ataendelea kuwemo ndani ya chama.
Malema amekuwa akiushambuliwa utawala Zuma mara kadhaa katika miezi ya hivi karibuni na kutaka serikali ya nchi jirani ya Botswana iondolewe madarakani.
Kama kijana huyo atapatikana na hatia, basi adhabu yake itakuwa kusimamishwa katika chama hicho kwa miezi kadhaa. ANC tayari ilikwisha sema itachunguza mashitaka hayo kwa ushirikiano wa timu ya watetezi ya Malema.
Hali hiyo itanyamazisha wito wake wa utaifa katika sekta ya madini, kutoa unafuu kwa wawekezaji, lakini pia itawakasirisha sana watu wanaomuunga mkono. Vijana wengine watano wanakabiliwa mashitaka kama hayo ya kinidhamu na yanatarajiwa kusikilizwa wiki ijayo.
Wanachumi wameonya kama Afrika Kusini itatekeleza mpango wa kutaifisha mali za wawekezaji, itatatengwa katika nyanja ya biashara za kimataifa na inaweza kufilisika.
Mwandishi: Sudi Mnette/ APE/RTR
Mhariri: Miraji Othman