1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mataifa yaliyoendelea duniani yapoteza imani na chanjo

Angela Mdungu
19 Juni 2019

Utafiti juu ya mienendo ya umma katika masuala ya afya duniani umeonesha kuwa watu wanaoishi kwenye nchi zenye uchumi mkubwa hasa barani Ulaya wamekuwa na imani ndogo katika chanjo dhidi ya magonjwa

https://p.dw.com/p/3KjHC
Symbolbild | Masernimpfungen
Picha: picture-alliance/dpa/empics/PA Wire/O. Humphreys

Matokeo ya utafiti huo, yanahusishwa na kuibuka kwa harakati dhidi ya chanjo ambapo watu hukataa kuamini faida za chanjo ama kudai kuwa ni hatari.

Ripoti ya shirika la masuala ya tiba ya Uingereza  iitwayo British medical Charity welcome trust, juu ya utafiti uliofanywa kati ya mwezi Aprili na mwezi Desemba mwaka uliopita, imeonesha kuwa Ufaransa inaongoza kwa kutokuwa na imani na chanjo. Ripoti hiyo imeonesha kuwa asilimia 33 ya raia wa Ufaransa hawakubaliani na kauli kwamba chanjo ni salama. Hata hivyo asilimia 79 ya watu duniani kote imeonesha kukubali kwamba chanjo ni salama huku asilimia 84 wakisema kuwa chanjo zinafanya kazi kwa ufanisi.

Ripoti hiyo imeonesha kuwa nchi za Bangladesh na Rwanda, zina imani kubwa na chanjo huku watu katika nchi hizo wakikubali kwa asilimia mia moja kuwa chanjo hizo ni salama na muhimu kwa watoto. Nchi zilizotajwa kuwa na imani ndogo zaidi na chanjo zimetajwa kuwa ni zile za Ulaya Magharibi zikifuatiwa na Ulaya Mashariki.

Ripoti ya shirika la Umoja wa Mataifa iliyotolewa mwezi Aprili mwaka huu ilionesha kuwa takribani watoto milioni 169 walikosa dozi muhimu ya kwanza ya chanjo dhidi ya surua kati ya mwaka 2010 na 2017. Kwa mujibu wa takwimu rasmi, kwa upande wa Marekani pekee, idadi ya visa vya ugonjwa huo kwa mwaka huu ni zaidi ya elfu moja.

Mosambik Beira | Impfkampagne gegen Cholera nach Überschwemmungen
Watoto wakisuburi kupatiwa chanjo dhidi ya kipindupindu MsumbijiPicha: picture-alliance/AP Photo/T. Mukwazhi

Nchi masikini ndizo zenye maambukizi zaidi

Mmoja wa wataalamu waliohusika kufanya utafiti huo, Imran Khan amesema kwa nchi ambazo watu wana imani kubwa na chanjo kama vile Misri na Bangladesh, ndipo kwenye magonjwa ya kuambukiza zaidi. Khan ameongeza kuwa kwa upande wa nchi zilizoendelea hata  ambapo mtu hapati chanjo, bado huwa katika hatari ndogo ya kupata maambukizi na kwamba hata mtu anapoambukizwa hapati matatizo makubwa ya kiafya kwani katika nchi hizo kuna mifumo mizuri ya afya.

Shirika la British medical Charity welcome trust la Uingereza lililofanya utafiti huo limesema linatumaini kuwa utafiti wake ni msingi mzuri kwa serikali mbalimbali duniani, kufuatilia jinsi tabia za watu zinavyobadilika hivyo kusaidia katika kutunga sera zinazolenga kutoa kinga, hasa  ugonjwa wa surua ambao haustahili kufumbiwa macho.

Kando na masuala ya chanjo, ripoti ya shirika hilo imeonesha pia kwamba, kuna tofauti za kijinsia katika ufahamu juu ya masuala ya kisayansi duniani ambapo asilimia 49 ya wanaume wamesema kuwa wanafahamu kiasi ama sana juu ya sayansi huku asilimia 38 pekee ya wanawake ndio waliokiri kuwa na ufahamu juu ya masuala hayo.