1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matokeo ya uchaguzi wa rais wa Gabon kutangazwa wakati wowote

Kabogo Grace Patricia2 Septemba 2009

Aidha, maafisa wa tume ya uchaguzi wamekutana kwa muda kabla ya kutangazwa matokeo hayo.

https://p.dw.com/p/JNv7
Maafisa wa uchaguzi wakihesabu kura za uchaguzi wa rais wa Gabon.Picha: AP

Nchini Gabon bado wakaazi wa taifa hilo wanasubiri matokeo yanayotarajiwa kutangazwa wakati wowote kutoka sasa. Wakati huo huo, maafisa wa tume ya uchaguzi nchini Gabon wamekutana kwa muda wa masaa kadhaa kabla ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi huo wa rais uliofanyika Jumapili iliyopita.

Mkutano huo ambao umeitishwa na tume hiyo ya uchaguzi, awali ulipangwa kufanyika asubuhi ya leo, lakini msemaji wa tume hiyo hakutoa sababu za kucheleweshwa huko. Kulikua na tetesi kwamba huenda muda wa kutangazwa kwa matokeo ya mrithi wa rais wa zamani wa nchi hiyo, Marehemu Omar Bongo Ondimba.

Aidha, haijafahamika iwapo tume hiyo ilikutana na wagombea wote 18 kama ilivyotangazwa hapo kabla.

Wagombea wakuu watatu katika kinyang'anyiro hicho cha urais, akiwemo mtoto wa rais Bongo, Ali Ben Bongo, wote wamedai kushinda uchaguzi huo, ambao uligubikwa na malalamiko ya kutofuatwa kwa kanuni za uchaguzi, japokuwa malalamiko hayo hayakuleta matukio ya ghasia.

Waangalizi wa Umoja wa Afrika katika uchaguzi huo, jana walisema kuwa wakati uchaguzi huo ulifata taratibu zote za kisheria, masanduku ya kupigia kura katika baadhi ya maeneo hayakufungwa na wafanyakazi katika baadhi ya vituo vya kupigia kura hawakuweza kuendesha vizuri utaratibu wa upigaji kura.

Ali Ben Bongo, waziri wa zamani wa ulinzi, anapewa nafasi kubwa ya kushinda uchaguzi huo na tayari amedai kushinda uchaguzi huo. Lakini wapinzani wake wakuu, Pierre Mamboundou na Andre Mba Obame, nao pia wamedai kushinda uchaguzi huo.

Pamoja na hayo wanazungumzia juu ya visa vya udanganyifu vilivyofanyika hata kabla ya uchaguzi. Miongoni mwa dosari zilizotajwa, walioorodheshwa kupiga kura ni karibu laki nane na nusu, wakati idadi ya wakaazi wa Gabon ni milioni moja na nusu.

Kwa wakati huu hali ni tete huku maduka yakiwa yamefungwa na wakaazi wengi wa mji mkuu wa Libraville wakiwa wameondoka kuelekea vijijini, huku Wizara ya ndani ikisema matokeo yatatangazwa leo usiku na mtu atakaye mrithi Marehemu Omar Bongo kujulikana.

Kiongozi huyo aliyeitawala nchi hiyo kwa miaka 41 na kufariki dunia Juni mwaka huu, ameacha kiasi watoto 30 na akaunti zaidi ya 66 za binafsi katika mabenki ya kigeni, huku Wagabon wakiendelea kuishi katika hali duni ya umasikini licha ya utajiri mkubwa wa mafuta wa nchi yao.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (AFP/APE)

Mhariri:M.Abdul-Rahman