Matumaini kwa Korea?
9 Agosti 2007Kwanza ni gazeti la “Volksstimme”, maana yake: Sauti ya Umma. Limeandika:
“Mkutano wa kwanza kati ya nchi hizo mbili za Korea mnamo mwaka 2000 umeimarisha sera ya mahusiano mazuri ya Korea Kusini kuelekea Korea Kaskazini. Lakini kama matumaini ya kuwa na umoja na amani yamekua haraka, vilevile yameharibika haraka pale Korea Kaskazini ilipoanza sera kali ya kinyuklia. Baada ya China kujitolea kupatanisha, serikali ya Korea Kaskazini imekubali kuachana na mradi wake wa kinyuklia ikipata msaada wa kiuchumi. Kwa hivyo, hali ikitulia ni nafasi nzuri kwa Korea Kusini kuanza upya mazungumzo na Korea Kaskazini ili kuimarisha usalama katika eneo hilo. Mkutano utakaofanyika, angalau, unaleta matumaini madogo.”
Ni gazeti la “Volksstimme”. Mhariri wa “Oldenburgische Zeitung” anakubali kuwa mazungumzo ya amani kati ya viongozi wa nchi hizo mbili za Korea ni ishara ya matumaini kwamba huenda Korea inaweza kuungana tena katika siku za usoni. Wakati huo huo, mhariri huyu anaonya:
“Kuna wasiwasi fulani kwamba kiongozi Kim Jong Il wa Korea Kaskazini, kwa kukubali mkutano na Korea Kusini, analenga kutatanisha mazungumzo na jumuiya ya kimataifa juu ya mradi wake wa kinyuklia. Huenda mkakati wake ni huo: Atalainisha masharti kwa kutishia kutokubali maafikiano na Korea Kusini.”
Na hatimaye juu ya suala hilo ni gazeti la “Handelsblatt” la mjini Düsseldorf:
“Hakuna mtu yeyote anayeweza kusema iwapo Korea Kaskazini kweli itatimiza ahadi zake. Mara nyingi tumeona vile serikali hiyo imebadilisha sera zake ghafla, ndiyo sababu haiaminiki. Hata hivyo, baada ya miaka mingi ya wasiwasi kuna matumaini tena katika nchi hii.”
Mada nyingine: Jana, baraza la mawaziri la Ujerumani lilikubali mabadiliko ya sheria inayohusu teknolojia ya visadifu. Kulingana na sheria hii mpya, shamba la maua yaliyobadilishwa kwenye visadifu lazima liwe mita 150 mbali na mashamba ya maua ya kawaida. Ikiwa ni mahindi, lakini umbali usiwe chini ya mita 300. Sheria hii inapingwa na wakulima na wanasayansi wengi. Vilevile wahariri wa magazeti wana wasiwasi, kama alivyoandika mwandishi wa gazeti la “Der neue Tag”:
“Sheria hii ni mwafaka mbaya, kwa sababu inajaribu kuthibiti jambo ambalo haliwezi kuthibitiwa. Haiwezekani kupanda maua ya kawaida na mengine yaliyobadilishiwa visadifu katika nchi moja bila ya athari. Mazingira hayajali sheria. Na hakuna kitu kama kubadilishwa kidogo visadifu, sawa na hakuna kitu kama kubeba mimba kidogo.”