Matumaini ya amani yeregea Congo
22 Septemba 2017Katika eneo kubwa la Kasai, mamlaka husika zimeanza kuandikisha wapiga kura ambayo ni shughuli muhimu sana kulipatia taifa hili utulivu.
Kulingana na kaimu gavana wa mkoa wa kati wa Kasai, Bwana Bernard Kambala Kamilolo, hilo linadhihirisha wazi kuwa amani imeanza kuonekana katika eneo hilo.
Huku ikiwa inakumbwa na umasikini na ufisadi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ni taifa kubwa ambalo limekuwa na historia ndefu ya vurugu haswa eneo la mashariki ambako hali imekuwa tete.
Eneo hilo la Kasai lenye utajiri wa almasi lilikuwa ni tulivu hadi mnamo mwezi Agosti mwaka wa 2016 pale kiongozi wa kikabila anayejulikana kama Kamwina Nsapu, ambaye alikuwa akipinga utawala wa Rais Joseph Kabila mjini Kinshasa na wawakilishi wake walipouawa.
Kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa, mapigano kati ya makundi ya kikabila na vikosi vya serikali yamesababisha vifo vya zaidi 3,000 na kiasi cha zaidi ya watu millioni moja kukimbia makwao.
Madai ya aina ya vurugu hizo ni pamoja na mauaji ya kiholela, ubakaji, mateso na utumizi wa askari watoto pamoja na uharibifu wa vijiji na mashule, majengo ya umma na kliniki.
Matumaini makubwa ni kwamba zoezi la usajili wa wapiga kura katika eneo la Kasai itafungua mlango wa kupatikana kwa suluhu wa mzozo wa kisiasa ulioko nchini Congo.
Maandalizi ya Uchaguzi Yaanza.
Taifa hilo lilitumbukia katika mgogoro mkubwa mwaka jana baada ya rais Kabila, tangu alipomrithi babake aliyeuawa mwaka wa 2001, kukatalia madarakani katika kile kilichokuwa kipindi chake cha mwisho kulingana na katiba ya taifa hilo.
Hata hivyo, makubaliano yaliafikiwa kati ya uongozi wa kabila na upinzani kufanyike uchaguzi mkuu mwishoni mwa mwaka huu wa 2017.
Lakini tarehe ya uchaguzi haijatangazwa hadi sasa na kunaonekana hakuna dalili ya kitu chochote kilichoahidiwa kwenye makubaliano hayo kutokea huku Rais Kabila akibakia mamlakani. Kati ya vikwazo vikubwa vya kufanyika kwa uchaguzi huo ni sintofahamu iliyopo katika eneo zima la Kasai japo mamlaka husika zimeweza kuandikisha wapiga kura millioni 42 katika mikoa mingine 24 ya taifa hilo.
Kuanza kwa zoezi la usajili wa wapiga kura jumanne kumeonyesha hamu kubwa ya wapiga kura ya kutaka utulivu.
Katika kituo cha usajili ndani ya shule ya kikatoliki katika eneo wilaya ya Kananga, foleni ndefu za watu zilijitokeza kwa hamu ya kupata kitambulisho. Katika wilaya ya Nganza ambayo ilikumbwa na machafuko, idadi ilikuwa ndogo sana ambapo kulingana na meya wa eneo hilo Mamie Kakubi, watu wengi wamelikimbia.
Hivyo wengi wana shiriki zoezi hilo kwa lengo la kufanya mabadiliko na kuimarisha hali nchini Congo. Kwa sasa hivi zoezi la usajili wa wapiga kura limeanza katika miji ya Kananga na Tshikapa mkoani Kasai. Watu bado wanaendelea kupewa mafunzo ya jinsi ya kuendesha utaratibu wa usajili huo na itachukua muda kupanua zoezi hili katika maeneo mengine.
Chini ya sheria, zoezi hilo la usajili wa wapigakura katika mkoa wa Kasai linafaa kuchukua muda wa siku 90 au miezi mitatu wakati ofisi ya usajili huo itakapofunguliwa. Hiyo inaathiri vibaya lengo la kuwa na uchaguzi mkuu mnamo Desemba 2017 kama ilivoafikiwa kwenye mkataba ulioandaliwa na kanisa katoliki ambalo lina ushawishi mkubwa japo haieleweki iwapo rais kabila ataheshimu makubaliano hayo.
Mwandishi: Fathiya Omar/AFP
Mhariri: Mohammed Khelef