1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matumaini yamezuka ya kufikiwa makubaliano katika mazungumzo ya Beijing kuhusu mradi wa kinuklea wa Korea ya kaskazini

27 Julai 2005
https://p.dw.com/p/CEqW

Beijing:

Mazungumzo ya pande sita yaliyolengwa kumaliza mvutano uliosababishwa na mradi wa kinuklea wa Korea ya kaskazini,yameingia siku yake ya pili hii leo mjini Beijing, mji mkuu wa jamhuri ya umma wa China.Hali jumla katika mazungumzo hayo yanayowaleta pamoja wawakilishi wa jamhuri mbili za Korea,jamhuri ya umma wa China,Marekani,Rashia na Japan, inaonyesha ni ya kutia moyo.Hata hivyo makubaliano hayatarajiwi katika duru hii ya nne ya mazungumzo .Msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje ya Marekani mjini Washington Sean McCormack amesema pengine duru mpya ya mazungumzo itahitajika.Duru tatu za mazungumzo zimeshafanyika tangu mzozo ulipozuka october mwaka 2002.Korea ya kaskazini iliyokiri mwezi february mwaka huu inamiliki nguvu za kinuklea,inaitaka Washington iachilie mbali siasa yake ya uadui,inalazimisha ipatiwe msaada wa kiuchumi, usalama wake udhamaniwe na itambuliwe kidiplomasia kabla ya kuachana na mradi wake wa kinuklia.Korea ya kusini imependekeza kuipatia Pyongyang nishati inayolingana na mahitaji jumla ya umeme ya Korea ya kaskazini.