1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mawaziri wa mambo ya nje wa EU wamjadili Trump

14 Novemba 2016

Mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya wamejadiliana mjini Brussels kuhusu mikakati endelevu kufuatia ushindi wa Donald Trump katika uchaguzi wa Marekani uliomalizika hivi majuzi.

https://p.dw.com/p/2Seiu
Belgien EU-Außenministertreffen in Brüssel
Picha: Reuters/Y. Herman

Mawaziri hao wamezungumzia kuhusu mbinu bora ambazo zitaweza kutumika katika kufikia makubaliano ya kibiashara, uhusiano na Urusi pamoja na kuhakikisha dhamira ya Marekani kuelekea Jumuiya ya Kujihami ya NATO yote hayo yakiwa ni mambo muhimu ambayo kwa sasa yamo katika mizani kufuatia ushindi wa Trump ambao haukuwa matarajio ya Umoja wa Ulaya. 

Mkutano huo ambao haukuwa rasmi umefanyika mjini Brussels ambapo mawaziri wa nchi za nje walijadili jukumu la Marekani katika maswala ya kisiasa ya Umoja wa Ulaya baada ya ushindi wa rais mteule wa Marekani Donald Trump wiki iliyopita.

Trump alizungumza mengi juu ya Umoja wa Ulaya wakati wa kampeni zake ambayo yamezigutusha nchi za umoja huo, kiongozi huyo aligusia kwenye hotuba za kampeni yake juu ya uwezekano wa Marekani kujiondoa kutoka kwenye ushirika wa NATO na kuzitaka nchi za Umoja wa Ulaya zijipangie zenyewe mikakati yake ya usalama huku akitumia wakati mwingi kumsifu rais Vladimir Puttin wa Urusi.

NATO: Marekani na Ulaya zahitajiana

Mkuu wa sera za Umoja wa Ulaya Federica Moghrerini amesema  "Kuna haja kwa watu wa Ulaya kuimarisha mikakati ya ulinzi, usalama na ushirikiano licha ya mabadiliko katika uongozi wa Marekani.  Ni muhimu tuzungumze na tufanye maamuzi sasa, huli lingekuwa angalizo kwa utawala wowote ule. Tuone utawala ujao utachukua hatua gani katika swala la ulinzi, hili litakuwa swala muhimu kwa siku za usoni na kwa vyovyote vile swala hili ni muhimu kwetu."  

Brüssel Brexit Gipfel Federica Mogherini
Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya Federica MogheriniPicha: Getty Images/AFP/P. Huguen

Wakati huo huo Bibi Mogherini amemshutumu waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Boris Johnson  ambaye hakuhudhuruia kikao hicho, ameifungamnisha hatua hiyo na kura ya maoni ya mwezi Juni ambapo raia wa Uingereza walipiga kura ya ndio kwa nchi yao kuweza kujiondoa kutoka kwenye Umoja wa Ulaya wenye nchi wanachama 28. Mogherini amesema hatua hiyo ya kujitoa kwenye umoja huo inaifanya Uingereza kuhitaji zaidi kuungwa mkono na Marekani katika makubaliano mapya ya kibiashara.

Wizara ya mambo ya nje ya Uingereza imekanusha shutma hizo na kutetea kutokuwepo kwa waziri wake wa katika kikao hicho. Taarifa hizo zimesema kuwa Uingereza haikuona sababu za muhimu za  kuhudhuria kikao hicho cha ziada na kwamba demokrasia imechukua mkondo wake na huku kipindi cha mpito kikiendelea Uingereza itafanya kazi na serikali ya Marekani ya sasa pamoja na ile itakayokuja ili mradi maslahi yake yatazingatiwa.  

Hii leo mawaziri hao wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya wanatazamiwa kufikia msimamo wa pamoja kuhusu Uturuki ambayo imekuwa ikiwaandama wapinzani wake pamoja na vyombo vya habari.

Mwandishi: Zainab AZIZ/ DPAE

Mhariri:Yusuf Saumu