Mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa ulaya wakutana Bruxelles
10 Machi 2008
Umoja wa Ulaya umeelezea matumaini kuona uchaguzi ujao wa bunge nchini Serbia ukigeuka kua kura bayana ya kuujongela Umoja wa Ulaya baada ya tangazo la uhuru la Kosovo.
Mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa mataifa 27 ya Umoja wa ulaya wanakutana mjini Bruxelles kuandaa mkutano wa kilele utakaofanyika alkhamisi na ijumaa ijayo .Mkutano huu wa mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa Umoja wa Ulaya umesadif pia baada ya waziri mkuu wa Serbia Vojislav Kostunica,mwenye kufuata siasa za wastani za kizalendo,kuivunja serikali ya muungano iliyodumu miezi kumi kati ya chama chake cha Democratic-DSS na vyama vyengine vinavyoelemea upande wa magharibi kikiwemo kile cha rais Boris Tadic cha serbia ya kidemokrasia DS.
Hitilafu za maoni miongoni mwa wanachama wa serikali hiyo ya muungano kuhusu Kosovo na uhusiano pamoja na umoja wa ulaya ndio chanzo cha kuvunjika serikali hiyo.Uchaguzi wa kabla ya wakati umepangwa kuitishwa May 11 ijayo.
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Slovenia,Dimitrij Rupel, ambae nchi yake ndio mwenyekiti wa zamu wa umoja wa ulaya,ameelezea haja ya kuviona vyama vinavyoelemea upande wa magharibi vikiibuka na ushindi.
Bwana Rupel anasema:
"Tunataraji ushindi utawaendea wale wanaoelemea upande wa Ulaya ya magharibi.Kuna ishara za kutia moyo.Makadirio ya maoni ya umma na maandamano ya wanafunzi.Kusema kweli sioni njia nyengine kwa marafiki zetu wa serbia isipokua kujiunga na Umoja wa Ulaya.Watakwenda wapi kwengineko?
Viongozi wa ulaya ambao mwezi uliopita walitoa mwito Boris Tadic achaguliwe upya kama rais wa Serbia, wamesema wazi kabisa wanauangalia uchaguzi mkuu ujao kama fursa mpya kwa waserbia kuwaarifu wanasiasa wao wanataka kujiunga na Umoja wa ulaya baada ya Kosovo kujitangazia uhuru wake.
Muakilishi mkuu wa siasa ya nje na usalama ya Umoja wa ulaya Javier Solana amesema tunanukuu: Waserbia wamejipatia fursa ya kuchagua mustakbal wao-mwisho wa kumnukuu.
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ufaransa Bernard Kouchner amewatolea mwito waserbia wautambue ukweli kwamba kanuni za zamani haziwezi tena kuendelezwa Kosovo na ndio maana wengi wa wanachama wa umoja wa Ulaya wameamua kuutambua uhuru wa eneo hilo.
Umoja wa ulaya umepitisha mkataba wa utulivu na ushirikiano pamoja na serikali ya mjini Belgrade,lakini unakwepa kuutia saini mkataba huo,unaoangaliwa kama hatua ya mwanzo kuelekea kujiunga Serbia na Umoja wa ulaya,kabla ya serikali ya mjini Belgrade kukubali kushirikiana kikamilifu na mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa vita vya Yugolslavia mjini The Hague nchini Uholanzi.
◄