Mawaziri wa Ujerumani wamekamilisha ziara Tanzania na kuelekea Afrika Kusini
9 Aprili 2010Waziri Westerwelle amesema hayo nchini Tanzania , kituo cha kwanza cha ziara yake ya siku tano barani Afrika.
Katika ziara yake, waziri wa mambo ya nje Guido Westerwelle anaongozana na waziri wa misaada ya maendeleo, Dirk Niebel.Hii ni ziara ya kwanza ya pamoja ya mawaziri hao barani Afrika.
Baada ya kuitembelea Tanzania leo watakuwa Afrika Kusini. Watamaliza ziara yao ya siku tano barani Afrika kwa kuitembelea Djibouti kwenye pembe ya Afrika.
Lengo la kutekeleza sera ya ufanisi zaidi ya mambo ya nje kwa makubaliano baina ya wizara hizo mbili limewekwa katika mkataba wa serikali ya mseto ya Ujerumani. Lengo hilo ni muhimu hasa kuhusu nchi zinazoendelea na zinazokabiliwa na migogoro ambapo wahisani na wadau wengine wanatekeleza ajenda tofauti.
Barani Afrika pana nchi nyingi kama hizo- vyombo vya habari kwa sasa vinaripoti sana hasa juu ya Somalia, nchi inayozingatiwa katika sera za nje za nchi za Ulaya na za Afrika kadhalika. Suala la Somalia pia limejadiliwa kwenye mazungumzo baina ya waziri Westerwelle na viongozi wa Tanzania.
Matukio ya sasa yanaonyesha jambo moja wazi: umaskini,migogoro katika ugavi wa raslimali,na maendeleo duni ni sababu zinazoweza kuchangia katika kuleta vurumai katika eneo zima.Uharamia unaotendeka kwenye pembe ya Afrika na Ghuba ya Aden ni miongoni mwa mifano.
Maharamia wanaziteka nyara meli ili kudai vitita vya fedha wanazotumia kwa ajili ya kugharimia vita vya nchini Somalia.
Mawaziri wa Ujerumani na wa Tanzania wameeleza wasiwasi wao juu ya mgogoro wa Somalia.
Waziri wa mambo ya nje wa Tanzania, Bernard Membe, amesema,
"Mizizi ya mgogoro wa Somalia hasa ni ya kiuchumi.Na tunatoa mwito kwa jumuiya ya kimataifa ihusiane na Somalia kama inavyohusiana na nchi nyingine ambamo migogoro inazuka. Nchi hizo zinahitaji usalama na mashirika yanayochangia katika kuleta mageuzi.Lakini asasi hizo zifanye kazi nchini Somalia, usalama utahitajika. Na hiyo ndiyo sababu tunatoa mwito kwa nchi zilizoahidi kuchangia askari zipeleke askari hao nchini Somalia. Nchi hizo ni pamoja na Nigeria, Ghana, Malawi na Senegal"Kwa upande wake, Tanzania ipo tayari kutoa mafunzo kwa polisi wa Somalia kwa msaada wa Ujerumani.
Mawaziri wa Tanzania na wa Ujerumani pia wamejadili suala la uharamia.
Waziri Westerwelle amesema harakati za kupambana na uharamia ni jambo la manufaa kwa wote.
"Ni kwa maslahi ya nchi zetu kuendesha harakati dhidi ya uharamia. Kwani sote tunategemea kuwepo kwa biashara huru duniani inayoleta manufaa kwa kila upande"Katika ziara yao ya siku tano barani Afrika mawaziri wa Ujerumani wa mambo ya nje, Guido Westerwelle, na wa ushirikiano wa maendeleo, Dirk Niebel, leo wameanza ziara nchini Afrika Kusini.
Mwandishi:Ute Schaeffer/Mtullya, Abdu
Mpitiaji: Miraji Othman