1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mawaziri wa zamani DRC wafungwa kwa ubadhirifu

Saleh Mwanamilongo
24 Machi 2020

Mawaziri wawili wa zamani akiwemo wa afya wamehukumiwa kwa kubadhiri fedha za umma zilizotakiwa kupambana na ugonjwa wa Ebola mashariki mwa nchi hiyo. Oly Ilunga amekutwa na hatia ya ubadhirifu wa dola laki nne.

https://p.dw.com/p/3Zxyz
Oly Ilunga waziri wazamani wa afya nchini Congo amehukumiwa miaka mitano jela
Oly Ilunga waziri wazamani wa afya nchini Congo amehukumiwa miaka mitano jelaPicha: AFP/Getty Images/F. Coffrini

Mawaziri wawili wa zamani akiwemo huyo wa afya wamehukumiwa mjini Kinshasa kwa kubadhiri fedha za umma.Oly Ilunga aliekuwa waziri wa faya nchini Congo amehukumiwa kifungo cha miaka mitano jela baada ya kukutwa na hatia ya ubadhirifu wa fedha za serikali zilizotakiwa kupambana na ugonjwa wa Ebola mashariki mwa nchi hiyo. Hata hivyo hukumu hiyo imezusha maswala mengi kuhusu vita dhidi ya rushwa ambavyo rais wa sasa Felix Tshisekedi aliweza kutangaza wakati alipochukuwa madaraka. 

Oly Ilunga aliyekuwa waziri wa afya hadi mwezi Julai amekutwa na hatia ya ubadhirifu wa dola laki nne ambazo zilitakiwa kutumika katika kupambana na ugonjwa wa Ebola huko mashariki mwa Congo kulingana na hukumu iliyotolewa na koti kuu mjini Kinshasa. Korti imemuhukumu Ilunga kifungo cha miaka mitano jela na kufanya kazi ngumu. Kwenye hukumu nyingine iliyotolewa na mahakama hiyo Guy Matondo aliyekuwa waziri wa fedha wa mji wa Kinshasa amehukumiwa kifungo cha miaka 8 ya kazi ngumu.

Katika taarifa aliyoitoa muda mfupi baada ya kutolewa hukumu dhidi yake, Oly Ilunga ametupilia mbali madai ya ubadhirifu wa fedha na kuelezea kwamba uamuzi wa koti kuu ulichochewa kisiasa. Aliendelea kusema kwamba hajawahi kuchukuwa fedha hizo zilizodaiwa kupotea na ameahidi kukata rufaa kwenye mahakama ya kimataifa, kwa sababu mahakama iliyowahukumu ni ya ngazi ya juu kabisa nchini Congo.

Je, ni ulipizaji kisasi ao  ni sheria inafata mkondo wake?

Korti kuu nchini Congo inaelezea kwamba dola laki nne zilizotakiwa kupambana na Ebola zilipotea
Korti kuu nchini Congo inaelezea kwamba dola laki nne zilizotakiwa kupambana na Ebola zilipoteaPicha: picture-alliance/AP Photo/J. Bompengo

Mashirika ya kutetea haki za binadamu ambayo yamepongeza kuweko na uamzi huo, lakini yamehoji utaratibu wa koti kuu katika kesi hiyo ambayo ilijaa na hisia nyingi za kisiasa. Kama anavyoelezea Omar Kavota wa shirika la kutetea haki za binadamau la CEPADHO.

''Sheria inapotendeka hakuna mtu alie juu ya sheria,lakini kutokana jitihada zake alizozifanya wakati alipokuwa waziri wa afya kwa ajili ya taifa la Congo hazingeweza pia kupuuzwa''. 

Kwa upande wake wakili wa Guy Matondo waziri wa zamani wa fedha amesema kwamba hukumu dhidi ya mteja wake ni ya kuchekesha.

Guy Matondo ametuhumiwa kwa ubadhirifu wa dola takriban milioni 22. Nchini Congo hukumu ya kazi ngumu haitekelezwi kwa hiyo wahukumiwa hao watabaki jela hadi kumalizika kwa kifungo chao.

Oly Ilunga aliyekuwa mtu wa karibu sana na daktari wa kipekee wa mpinzani Etienne Tshisekedi baba wa rais wa sasa Felix Tshisekedi alikubali kufanya kazi na rais wa zamani Joseph Kabila, kama waziri wa afya, katika serikali ya umoja wa kitaifa iliyoundwa mwaka 2016.

Uhusiano ulikuwa mbaya baina ya Oly Ilunga na rais Felix Tshisekedi baada ya Tshisekedi kuchukuwa madaraka, na kusababisha kujiuzulu waziri Ilunga mwezi Julai mwaka uliopita. Alifunguliwa mashtaka ya ubadhirifu wa fedha siku chache tu baada ya kujiuzulu kwake.