Mazungumzo ya Amani ya Sudan Addis Abeba
14 Februari 2014Katika ufunguzi wa mazungumzo hayo yanayosimamiwa na Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa,ya kwanza ya aina yake tangu mwezi April mwaka jana,serikali ya mjini Khartoum imesema imedhamiriia kuona matumizi ya nguvu yanakoma.
"Tunahudhuiria mazungumzo kwa lengo la kufikia amani itakayowaokoa wananchi wetu toka janga la vita na maangamizi" amesema kiongozi wa ujumbe wa Khartoum katika mazungumzo hayo Ibrahim Ghandour..
Lakini chama hasimu -Vuguvugu la Ukombozi wa wananchi wa Sudan Kaskazini-SPLM-N wanashuku dhamiri halisi za serikali na kuituhumu kufanya mashambulio ya angani na kuzuwia misaada ya kiutu.
"Mengi yanasemwa na viongozi wa Khartoum wanaodai wanataka mageuzi-tutauona ukweli leo" amesema kwa upande wake kiongozi wa ujumbe wa SPLM-N Yassir Arman katika mahojiano na shirika la habari la Ufaransa-AFP.
Amani ndio Ufunguo wa Maendeleo
Mpatanishi wa Umoja wa Afrika,rais wa zamani wa Afrika Kusini Thabo Mbeki amehakikisha pande zote mbili zitasalia mjini Addis Ababa hadi makubaliano yatakapofikiwa."
Mazungumzo haya yanaitishwa baada ya umoja wa mataifa kuihimiza serikali ya mjini Khartoum na waasi waweke chini haraka silaha ili kuruhusu misaada ya kiutu iwafikie raia zaidi ya milioni moja wanaosumbuliwa na vita.
"Pande zote mbili katika meza ya mazungumzo zinatakiwa zitangaze moja kwa moja mwisho wa uadui na kuruhusu watumishi wa mashirika ya misaada ya kiutu wasambaze misaada inayohitajika katika maeneo ya mapigano" amesema mkuu wa tume ya Umoja wa mataifa nchini Sudan Ali Al-Zaatari.
Katika wakati ambapo pande hizo mbili zinakutana katika mji mkuu wa Ethiopia-Addis Ababa mashambulio ya vikosi vya serikali ya mjini Khartoum yameendelea-hayo lakini ni kwa mujibu wa muasisi wa mtandao wa Nuba Reports,Ryan Boyette wenye makao yake Kordofan Kusini.Boyette anasema ndege ya kijeshi chapa Sukhoi imevurumisha mabomu kadhaa katika shule moja jana jioni na mengine kadhaa karibu na mahala mifugo inakokwenda kunywa maji."
"Hatutupi mabomu katika maeneo wanakoishi raia" amekanusha msemaji wa jeshi Sawarmi Khaled Saad na kuongeza tunanukuu" jeshi litaendelea na kazi yake hadi makubaliano ya kuweka chini silaha yatakapofikiwa."Mwisho wa kumnukuu.
Idadi halisi ya wahanga wa mapigano ya miaka mitatu katika jimbo la Kordofan Kaskazini na Blue Nile haijulikani.
Umoja wa Mataifa unakadiria watu milioni moja na laki mbili wameyapa kisogo maskani yao au kusumbuliwa na mapigano katika maeneo hayo mawili yanayopakana na Sudan Kusini.
Mazungumzo ya Addis Ababa yanasadif wiki mbili baada ya rais Omar el Bashir kutoa wito wa kuanzishwa enzi mpya ya kisiasa na kiuchumi-amani ikiwa kipa umbele.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP
Mhariri:Yusuf Saumu