1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mbabe wa vita wa DR Kongo ahukumiwa kifungo cha maisha

Yusra Buwayhid
24 Novemba 2020

Mbabe wa zamani wa kivita katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amehukumiwa kifungo cha maisha kwa makosa ya uhalifu dhidi ya binadamu, pamoja na ubakaji wa watu wengi.

https://p.dw.com/p/3lkU9
Prozess in Goma
Picha: Jonas Gerding

Mahakama ya kijeshi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Jumanne imemhukumu kifungo cha maisha mbabe wa kivita Ntabo Ntaberi Sheka baada ya kumkuta na hatia ya makosa kadhaa ikiwa ni pamoja na uhalifu wa kivita, mauaji, ubakaji, utumwa wa ngono, na kuwatumia watoto kama wanajeshi nchini humo.

Kesi hiyo iliyosikilizwa kwa takriban miaka miwili, na kuwahusisha zaidi ya wahanga 300 ni ya kihistoria katika harakati za kusaka haki nchini humo kulingana na makundi ya kutetea haki za binadamu pamoja na Umoja wa Mataifa.

"Eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo halijawahi kushuhudia kesi ya kiwango kama hiki. Kwa hali yoyote, hili ni tukio la kihistoria," amesema Elsa Taquet ni mshauri wa masuala ya sheria wa TRIAL International, shirika lisilo la kiserikali linalopambana na uhalifu wa kimataifa na kusaidia wahanga katika harakati za kusaka haki zao.

"Sheka amepatikana na hatia ya uhalifu wa kivita, na ni mtu ambaye hakuna aliedhani angewahi kumuona amepandishwa kizimbani, kwa hivyo hii ni hatua kubwa kwenye suala la haki," amesema Taquet .

Sheka alianzisha kundi la wanamgambo la Nduma Defence of Congo (NDC) katika jimbo la Kivu Kaskazini, ambako alidai walikuwa wakipambana na waasi wa Kihutu wa Rwanda wa FDLR.

Prozess in Goma
Mahakama ya kijeshi Goma ikisikiliza kesi ya Ntabo Ntaberi ShekaPicha: Jonas Gerding

Wahanga walioonyesha ujasiri

Waranti wa kukamatwa kwake ulitolewa mnamo Januari 2011 kufuatia mashambulizi kadhaa ya kundi la NDC na makundi mengine mawili ya wanamgambo yanayodaiwa kuwabaka takriban watu 400 katika vijiji 13 kati ya Julai 30 na Agosti 2, mwaka 2010.

Tangu wakati huo, Sheka aliendelea kusakwa hadi mwaka 2017, alipojisalimisha kwa askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa.

Daniele Perissi, mwakilishi wa shirika hilo la TRIAL International, amesema mamlaka zimethibitisha kuwa zina uwezo wa kushughulikia kesi ngumu sana na kutoa kuhumu inayostahili kwa mtazamo wa kisheria.

Sheka na Séraphin Zitonda, mbabe wa kivita kutoka kundi lingine la wanamgambo, walihukumiwa kifungo cha maisha jela katika kesi hiyo iliyosikilizwa mjini Goma, kwa uhalifu uliofanywa katika jimbo la Kivu Kaskazini mashariki mwa Kongo kati ya mwaka 2010 na 2014.

"Nawapongeza wateja wake kwa kuonyesha ujasiri wa hali ya juu na kuendelea kutoa ushahidi licha ya vitisho walivyokuwa wakikabiliana navyo," amesema Yuma Fatuma Kahindo, mwanasheria aliyewakilisha kundi la wahanga wa uhalifu huo.

Jeshi nalo limesema litaendelea na hatua za kuhakikisha haki inatendeka dhidi ya watu waliodhulumiwa.

Vyanzo: (rtre,afptv)