1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mchakamchaka wa kumpata kiongozi mpya wa ANC waanza.

Siraj Kalyango4 Desemba 2007

Kampeini zatishia kukigawanya chama

https://p.dw.com/p/CX6w
Rais Thabo Mbeki wa Afrika Kusini,kulia akisalimiana na rais Mugabe wa Zimbawe,kushoto.Mvutano kati ya Mbeki na Jacob Zuma kukiongoza chama tawala cha African National congress- ANC watishia kukisambaratishaPicha: AP

Harakati za kutafuta kiongozi wa chama tawala nchini Afrika kusini unapamba moto. Hata hivyo mbio za kumtafuta kiongozi mpya wa chama cha African national Congress-ANC- zinatishia kukisambaratisha chama hicho.

Chama tawala na cha watu waliowengi nchini Afrika kusini –ANC-kinaelekea kugawanyika.Hii ni kutokana na kung’agang’ania madaraka wa chama hicho.Mg’ang’anio ulioko sasa, ambao hauna mwongozo wa waasisi wa chama,waweza ukakiletea mashaka hapo mbeleni.

ANC kinafanya uchaguzi wa wakuu wa chama mwezi huu katika mkutano mkuu utakaofanyika kuanzia taerehe 16 hadi 20.

Mkutano huo utafanyika baada ya kutokea mgawanyiko wa wanachama.Sasa kumejitokeza makundi mawili.Moja la liko nyuma ya rais wa sasa wa nchi hiyo ambae pia anashikilia bendera ya kiongozi wa chama-Thabu Mbeki.Kundi lingine linamuunga mkono naibu wake chamani- Jacob Zuma.

Mvutano kati ya vigogo hao wawili, unatishia harakati za kuundwa kwa sera ya kupambana dhidi ya umaskani, UKIMWI pamoja visa vya uvunjaji wa sheria.

Mvutano huu unaweza ukaamua nani ataekalia kiti cha kiongozi wa nchi hiyo wa hapo baadae.

Wadadisi wa masuala ya kisiasa wanasema,mvutano huo, unaweza ukatishia mustakbala wa chama hicho kwa kuongeza zaidi tofauti zilizoko.Wengine wamependekeza kuwa vigogo wote wawili inafaa wajiondoe katika mbio hizo na kumuachia mmoja mwingine ambae anaonekana anakiunganisha chama.

Ingawa tofauti za awali ziliweza kutanzuliwa wakati wazee wa chama walipoingilia kati ,mara hii wachache waliobaki kufanya hilo.

Mzee Nelson Mandela, ambae ni alama ya usuluhishi na aliekiongoza chama ANC kupata ushindi,katika uchaguzi wa kwanza ulioshirikisha watu wote bila kujali rangi zao, mwaka wa 1994, ameacha masuala ya siasa.

Vyombo vya habari nchini Afrika kusini vinaripoti kuwa hata wakfu wa Mandela uliliondoa tangazo la tuzo la Nobel- linalomuonyesha Mzee Mandela akiwa na Bw Mbeki.Inasemekana kuwa hatua hiyo ilifanywa kwa hofu kuwa itaonekana kama Mzee anamuunga mkono mtu fulani.

Na wazee wengine, nguzo muhimu za Chama hicho waliopigania chama kufa na kupona , ndani na nje ya nchi-Walter Sisulu na Oliver Tambo, sasa ni marehemu.

Ikiwa Bw Zuma atashinda na kuchukua uongozi wa ANC, kama anavyotarajiwa na wengi, bila shaka atakuwa rais wa nchi.

Jambo hilo litakuwa pigo kubwa kwa Bw Mbeki ambae angetaka ushawishi wake katika siasa za nchi uendelee hasa katika kumbariki mtu atakaemrithi wakati muhula wake utakapomalizika mwaka wa 2009.

Mbeki na Zuma,waliachana mwaka wa 2005 wakati Zuma alipofutwa kazi kama makamu wa rais wa nchi, kufuatia shutuma za kuhusishwa katika kesi ya ulanguzi. Wafuasi wa Zuma walidai kuwa mtu wao alisingiziwa na hizo zikikuwa njama za kisiasa zinazofanywa na watu wanaomuunga mkono Mbeki.

Tofauti zao zimekilazimisha chama kuegemea upande na tofauti hizo zimejitokeza mno wakati wa kampeini.

Mbeki anaungwa mkono na wafanya biashara,ilhali Zuma yeye anashabikiwa na vyama vya wafanyakazi.

Hali hii si mpya kukikumba chama hicho.Katika miaka ya 70 baadhi ya wakereketwa wa chama hicho walijitenga na kudai kumfuta kazi kama kiongozi,Oliver Tambo.Walimteua Mandela ambae alikuwa gerezani kuwa kiongozi wao.Aliuzima uasi huo kwa kukataa uongozi akisema alikuwa baado anamtambua Tambo.

Na katika mkutano wa kwanza wa kitaifa wa chama hicho,baada ya kuondoka uhamishoni mwaka wa 1991,Mbeki na Chris Hani walionekana kama waliokuwa mstari wa mbele kuchukua nafasi ya unaibu mkuu wa chama.Ili kuepuka mgawanyiko,Sisulu alishawishiwa kusimama. Baadae Hani ,aliekuwa kiongozi wa chama cha kikomunisti cha Afrika kusini, aliuawa kwa kupigwa risasi mwaka wa 1993, nae Sisulu alijiondoa na kumuachia Mbeki.

Je na mara hii, chama cha ANC kitanusurika na mgawanyiko kama nyakati zilizopita.Hayo yataweza kufahamika baada ya matokeo ya mkutano mkuu wa baadae mwezi huu.