Mechi za Ligi ya Mabingwa Ulaya zarejea
2 Oktoba 2012Klabu ya Bayern Munich itakuwa bila ya kiungo Mholanzi Arjen Robben katika mchuano wao wa kesho wa ligi ya mabingwa Ulaya nchini Belarus dhidi ya klabu ya BATE Borisov kesho Jumanne.
Robben alikosa mchuano Jumamosi wa Bundesliga ambapo waliishinda Werder Bremen magoli mawili kwa sifuri. Afisa mkuu mtendaji wa Bayrn, Karl-Heinz Rummenige alisema anataraji kuwa Bayern wataendelea na mwanzo wao mzuri msimu huu katika mchuano huo wao wa kwanza ugenini katika ligi ya mabingwa Ulaya.
Washindi mara saba wa kombe hilo AC Milan itapambana na Zenit St Petersburg Jumatano huku wakiwa wameshinda moja tu kati ya mechi zai 11 za mwisho ugenini katika ligi ya mabingwa. Nao mabingwa watetezi Chelsea wanataraji kutoka nchini Denmark na pointi zote tatu watakapocheza kesho na klabu ya Nordsjaelland. Klabu hiyo ndogo ambayo inacheza kwa mara ya kwanza ligi ya mabingwa, ilishindwa mbili bila jawabu na Shaktar Donestk katika mchuano wa kwanza.
Manchester City watakuwa nyumbani kuchuana na mabingwa wa Ujerumani Borussia Dortmund katika mechi ya kundi D. baada ya kukubali kufungwa magoli mawili katka dakika za mwisho mwisho ambayo yaliipa Madrid ushindi wa mabao matatu kwa mawili, City watajitahidi kuendeleza rekodi yao ya kutoshindwa mechi 17 za Ulaya ilizocheza nyumbani. Dortmund iliwashinda Borussia Moenchengladbach magoli matano kwa moja mwishoni mwa wiki.
Ajax Amsterdam itapambana na Real Madrid. Timu hizo zimekutana katika awamu ya makundi katika misimu miwili iliyopita ya ligi ya mabingwa huku Real ikishinda mechi zote nne na kufunga magoli 12 bila kufungwa hata moja. Arsenal watakuwa nyumbani Emirates kuialika Olympiakos katika mchuano wa kundi B. timu hizo mbili zinakutana katika awamu ya makundi kwa mara ya tatu katika misimu minne.
Barcelona wanalenga kupiga hatua kubwa katika barabara ya kuelekea katika awamu ya maondowano kwa kusajili wa pili mfululizo wakati watakapozuru nyumbani kwa Benfica kesho, siku tano kabla ya kuchuana na mchuano mkali dhidi ya mahasimu wake wa La Liga Real Madrid.
Barcelona iliendeleza mwanzo bora wa msimu kwa kutoka nyuma na kuishinda Sevilla magoli matatu kwa mawili Jumamosi katika mchuano wa La Liga. Barca wamepigwa jeki na kurejea kwa mshindi wa taji la Ballon D'Or Andres Iniesta na nahodha Crles Puyol. Nayo Spatark Moscow watawaalika Celtic katika mchuano mwengine wa kundi C.
Katika mchuano mwingine Juventus haijashindwa msimu huu na inaingia katika mchuano wao wa kwanza wa nyumbani katika ligi ya mabingwa, dhidi ya Shaktar Donetsk, timu ambayo imeshinda mechi zake zote za mwanzo 13. mwishoni mwa wiki Juve ilishinda Roma magoli manne kwa moja.
Mshambuliaji wa klabu ya Manchester City, Muargentina Sergio Aguero amewasbutumu waamuzi wa Uingereza kwa ubaguzi dhidi ya wachezaji wa kigeni katika mechi za ligi kuu.
Aguero ambaye alifunga bao lake la kwanza msimu huu na kusawazishia Manchester City ambayo iliifunga Fulham mabao mawili kwa moja siku ya Jumamosi, alisema marefa wanawabagua wachezaji wa kigeni na kuwapuuza wakati wa malalamiko ya penalti.
Alisema pia wachezaji wa kigeni huadhibiwa sana kwa penalty ambazo hazifai kupewa dhidi yao. Wenzake Pablo Zabaleta na Carlos Tevez walinyimwa penalty katika mchuano huo. Mkufunzi wake Roberto Mancini pia alikosoa uamuz wa penalty iliyofungwa na mchezaji wa Fulham Mladen Petric.
Matukio mengine yanayowahusisha wachezaji wa kigeni yaliibua wasiwasi Jumamosi. Beki wa Chelsea David Luiz alipewa kadi ya njano kwa kupiga mbizi wakati Chelsea ilipoishinda Arsenal magoli mawili kwa moja. Lakini beki wa Gunners Muingereza Carl Jenkinson, ambaye alijifanya kujiangusha.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/Reuters/DPA
Mhariri: Yusuf Saumu