Merkel apinga kuifunga njia ya Balkan kwa wahamiaji
7 Machi 2016Waziri mkuu wa Uturuki Ahmet Davutoglu alisema mkutano huo utazingatia azma ya Uturuki kujiunga na umoja wa Ulaya na ana matumaini utakuwa wa umuhimu mkubwa katika kulifikia lengo hilo. Huku maelfu ya wakimbizi wakiwa wamekwama nchini Ugiriki kutokana na mipaka kufungwa, mkutano huo huenda ukatangaza rasmi kuifunga njia ya Balkan kutoka Ugiriki hadi Ujerumani, ingawa hilo ni mojawapo ya masuala yaliyosababisha tofauti kubwa ya maoni.
Viongozi wataahidi kuisaidia Ugiriki kukabiliana na wimbi la wahamiaji na kupata hakikisho kwamba Uturuki kwa msaada wa jumuiya ya kujihami ya NATO, itawazuia wafanyabiashara kuwasafirisha wahamiaji kupitia baharini.
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel alisema anapinga wazo la kuifunga mipaka akisema ana matumaini kutapatikana muafaka katika mkutano wa leo. "Hii ina maana tutajadiliana vipi tunavyoweza kuondosha sababu za wimbi la wakimbizi; tunavyoweza kuilinda mipaka yetu ili kuboresha hali kwa nchi zote, na natumai kwa malengo haya tutaafikiana leo, lakini yatakuwa mazungumzo magumu."
Merkel na waziri mkuu wa Uholanzi, Mark Rutte, ambaye nchi yake inashikilia urais wa kuzunguka wa Umoja wa Ulaya, walikutana kwa muda wa masaa matano na Davutoglu mjini Brussels, kujaribu kumshawishi kiongozi huyo akubali kukomesha wimbi la wakimbizi baada ya zaidi ya watu milioni moja, wengi wakiwa raia wa Syria, Iraq na Afghanistan, kuingia Ulaya mwaka uliopita, wengi wao wakifikia Ujerumani.
Uturuki yawasilisha mapendekezo mapya
Akizungumza leo alipowasili katika afisi za baraza la Ulaya kunakofanyika mkutano Davutoglu alisema, "Nina hakika changamoto hizi zitatatuliwa kupitia ushirikiano na Uturuki iko tayari kushirikiana na Umoja wa Ulaya. Uturuki iko tayari kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya pia na leo natumai mkutano huu utakuwa wa ufanisi na hatua muhimu katika mahusiano yetu kwa njia chanya."
Maafisa wa Ulaya walisema Davutoglu ametia munda kwa kutaka fedha zaidi kutoka kwa Umoja wa Ulaya mbali na dola bilioni tatu zilizoahidiwa na umoja huo kuwasaidia wakimbizi milioni 2.9 kutoka Syria ambao Uturuki inawahudumia. Uturuki imetaka pia mazungumzo juu ya ombi lake kutaka kujiunga na Umoja wa Ulaya yaharakishwe na sheria kuhusu visa za kusafiria katika nchi wanachama wa umoja huo zilegezwe mara moja kwa Waturuki, mapendekezo mapya ambayo yamesababisha mkutano huo wa nusu siku kurefushwa.
Viongozi wa Ulaya pia walielezea wasiwasi wao kwamba ushirikiano na Uturuki unasadifiana na ukandamizaji wa uhuru wa vyombo vya habari ambao ni kinyume na maadili ya Ulaya. Rais wa Ufaransa Francois Hollande aliutaka Umoja wa Ulaya uendelee kuwa chonjo kuulinda uhuru wa vyombo vya habari nchini Uturuki licha ya mahitaji yake ya ushirikiano na taifa hilo katika kupunguza wimbi la wakimbizi barani Ulaya.
Mwandishi:Josephat Charo/rtre/dpae/
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman