1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel kukutana na Waziri Mkuu wa Uturuki

15 Februari 2018

Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel leo anakutana na Waziri Mkuu wa Uturuki, Binali Yildirim mjini Berlin, katika juhudi za kurejesha uhusiano wa kirafiki baada ya nchi hizo kuwa kwenye mzozo kwa zaidi ya mwaka mmoja.

https://p.dw.com/p/2sjGc
Türkei  Angela Merkel - Binali Yildirim
Picha: Reuters/Ho

Mazungumzo ya viongozi hao wawili yanatarajiwa kutawaliwa zaidi na hatua ya kushikiliwa kwa mwanadishi habari wa Ujerumani mwenye asili ya Uturuki, Deniz Yuecel bila ya kufikishwa mahakamani.

Katika mahojiano na kituo cha televisheni cha Ujerumani, ARD, yaliyorushwa jana, Yildirim alisisitiza kuwa uamuzi wa iwapo mwandishi huyo wa gazeti la Die Welt ataachiwa huru au la, huenda ukachukuliwa na majaji wa Uturuki na sio serikali yake.

''Jambo hilo ni la kikatiba. Mimi siwezi kutoa uamuzi huu. Mahakama ndiyo inafanya maamuzi. Nina matumaini kwamba ataachiwa huru hivi karibuni. Na nadhani kwamba mafanikio yatapatikana katika kipindi kifupi kijacho,'' alisema Yildirim.

Yuecel, mwenye umri wa miaka 44 alikamatwa mwaka mmoja uliopita mjini Istanbul na amekuwa kizuizini kwa makosa ya kujihusisha na ugaidi, lakini tangu wakati huo waendesha mashtaka wa serikali bado hawajamfunguliwa mashtaka yoyote rasmi ya uhalifu.

Mada zitakazojadiliwa

Kabla ya ziara yake, Yildirim alisema katika mkutano wake na Merkel watazungumzia uhusiano kati ya Uturuki na Umoja wa Ulaya, biashara kati ya nchi hizo mbili, raia milioni 3.5 wa Uturuki wanaoishi nchini Ujerumani, pamoja na harakati za kizalendo barani Ulaya.

Journalist Deniz Yücel
Mwandishi habari, Deniz YuecelPicha: picture-alliance/Eventpress/Stauffenberg

Katika miaka ya hivi karibuni uhusiano kati ya Ujerumani na Uturuki uliharibika kutokana na kile ambacho Ujerumani inakiona kama kuongezeka kwa utawala wa kimabavu wa Rais Recep Tayyip Erdogan, ambaye aliongezewa mamlaka zaidi katika kura ya maoni yenye utata iliyofanyika mwaka uliopita.

Hata hivyo, Yildirim amesema kipindi hicho kimepita. Aidha, amesema msimamo wa Ujerumani kuhusu shughuli zinazofanywa na chama cha Wafanyakazi wa Kikurdi, PKK ambacho kimepigwa marufuku, kwa sasa unaridhisha. Pia uhusiano kati ya washirika hao wawili wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO umeanza kuimarika baada ya Uturuki kuwaachia huru raia kadhaa wa Ujerumani.

Siku ya Jumatatu, msemaji wa Kansela Merkel, alisema kuwa kisa cha Yuecel na Wajerumani wengeni wanaoshikiliwa Uturuki kwa sababu za kisiasa, kinaufanya uhusiano kati ya nchi hizo mbili kuwa mbaya. Katika kipindi chote cha mwaka uliopita, Merkel alisema wazi kwamba anatarajia Uturuki itawaachia huru raia wa Ujerumani ambao wanashikiliwa Uturuki kwa kutokuzingatia haki.

Jana, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Sigmar Gabriel alisema baada ya kujadiliana mara kwa mara kuhusu kisa cha Yucel na waziri mwenzake, Mevlut Cavusoglu, ana matumaini uamuzi mzuri kuhusu Yucel utafikiwa hivi karibuni na mahakama huru ya Uturuki.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/DPA, AFP
Mhariri: Josephat Charo