Merz akemea kauli za Musk kuunga mkono AfD Ujerumani
30 Desemba 2024Mwanasiasa wa kihafidhina anayetaka kuwa kansela ajaye wa Ujerumani, Friedrich Merz, amemkemea bilionea wa sekta ya teknolojia nchini Marekani Elon Musk kwa kukiunga mkono chama cha siasa kali za mrengo wa kulia kinachojiita chama Mbadala kwa Ujerumani - AfD katika uchaguzi ujao. Merz ambaye ni mkuu wa chama cha Christian Democratic Union - CDU amesema hawezi kukumbuka, katika historia ya mataifa ya Magharibi, kwamba kumekuweko na kisa cha kufananishwa cha uingiliaji kati kampeni ya uchaguzi ya nchi rafiki. Merz ameutaja wito wa Musk wa kuiunga mkono AfD katika uchaguzi wa Februari 23 kuwa ni usumbufu unaopindukia. Katika maoni aliyoandika kwenye gazeti la kihafidhina la Ujerumani Die Welt, Musk alikielezea chama chama cha AfD kuwa ndio cheche ya mwisho ya matumaini kwa Ujerumani. Makala hiyo ilisababisha kujiuzulu kwa mhariri mmoja mwandamizi wa gazeti hilo.