Miaka 10 ya wimbi la mapinduzi ya Uarabuni
8 Desemba 2020Miaka kumi iliyopita, mamilioni ya watu walithubutu kuwa na ndoto ya mabadiliko ya kisiasa na kuingia mitaani kwenye miji mikubwa ya mataifa ya Kiarabu kuanzia kaskazini mwa Afrika, Mashariki ya Kati hadi Ghuba ya Uajemi.
Hivi sasa, muongo mmoja baadaye, maelfu yao wanaozoea kwenye magereza wakikabiliana na mateso ya kikatili, na matumaini yao yameyeyuka kama moshi angani.
Kutoka Cairo hadi Damascus, tawala zimefanikiwa kuuangamiza upinzani ulioibua mwanzoni mwa kile kilichokuja kujuilikana kama Machipuko ya Arabuni, ambapo sasa waandamanaji wengi nchini Syria na Misri wamenyamazishwa kupitia mateso na vifungo, na hata wengine kwa vifo.
Kwa mujibu wa mashirika mbalimbali ya haki za binaadamu, nchini Misri pekee kufikia sasa kuna wafungwa 60,000 wa kisiasa, ambao ni matokeo ya wimbi hilo la mageuzi lililofanikiwa kumng'oa madarakani dikteta Hosni Mubarak mwanzoni mwa mwaka 2011.
Ripoti ya shirika la Amnesty Interenational ya mwaka 2018 iliitaja Misri, taifa la watu milioni 100, kama "gereza la wazi kwa wakosoaji wa serikali." Wiki moja tu iliyopita, shirika hilo lililaani vikali mauaji ya kiholela ambapo watu 57 wameuawa ndani ya miezi miwili tu iliyopita, ambayo ni takribani mara ya mbili ya wale waliouawa mwaka jana.
Nchini Syria, ambako vita vya kikatili vya wenyewe kwa wenyewe vingali vinaendelea na ambavyo tayari vimeshaangamiza maisha ya watu zaidi ya 380,000, mahabusu wanaendelea kukumbana na mauti yao wakiwa vizuizini.
Mwaka 2017, Amnesty International ilisema kuwa serikali ya Rais Bashar al-Assad imekuwa ikitumia mbinu ya utesaji na kuwapoteza watu wasijulikane walipo kama njia ya kupambana na upinzani dhidi yake kwa miongo kadhaa sasa.
Lakini ukatili huo umeongezeka maradufu tangu mwaka 2011, ambapo shirika la Human Rights Data Analysis linasema kuwa watu 17,723 waliuawa ndani ya mahabusu za serikali baina ya mwaka 2011 na Disemba 2015, ikimaanisha kuwa watu 300 walikuwa wakiuliwa kila mwezi.
Hata hivyo, idadi iliyokusanywa na shirika la uangalizi wa haki za binaadamu la Syria lenye makao yake London, Uingereza, inaonesha kuwa waliouawa magerezani nchini Syria ni zaidi ya 100,000 tangu mwaka 2011.
Lakini serikali za Misri na Syria zimekuwa zikikanusha tuhuma hizo na badala yake kuyashutumu makundi ya haki za binaadamu kwa kuelemea upande mmoja na kuingilia mambo yao ya ndani.
Na kwa kuwa ndani ya harakati za amani za umma kubadilisha tawala zao kwa maandamano ya mitaani kulijipenyeza makundi ya siasa kali, serikali hizo zimekuwa zikihalalisha matumizi yao ya nguvu na mbinu za kikatili kuwa ni sehemu ya vita vya kilimwengu dhidi ya makundi ya kigaidi.
Taarifa kuhsu wafungwa daima ni chache na haba mno kupatikana, na familia zao kawaida hutumia miaka kadhaa kuwasaka watoto wao. Ilichukuwa miaka zaidi ya saba kwa familia nyingi nchini Syria kuja kutambuwa mwaka 2018 kwamba kumbe wapendwa wao walikuwa wameshakufa miaka kadhaa nyuma, baada ya serikali kutoa orodha mpya ya rikodi za vifo.
Mmoja wao ni Salwa, ambaye baada ya kukaa miaka saba bila taarifa yoyote kuhusu mpwa wake aliyekamatwa kwenye maandamano ya mwaka 2011, alikuja kuambiwa mwaka 2018 kwamba kumbe alikuwa amekufa tangu miaka mitano iliyopita.
"Hata kwenye kuomboleza, tunaogopa kuonesha majonzi yetu, na hujifanya kuwa ni kudura ya Mungu tu imepita," anasema Salwa.