1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miaka 50 tangu maandamano makubwa ya wanawake nchini Afrika Kusini

Dagmar Wittek / Maja Dreyer9 Agosti 2006

Leo imetimia miaka hamsini tangu wanawake 20.000 wa Afrika Kusini walipoandamana dhidi ya sheria za ubaguzi wa rangi zilizopitishwa na serikali ya utawala wa kibaguzi wa nchi hiyo wakati huo. Mwandishi wetu wa Afrika Kusini, Dagmar Wittek, amekutana na mwanamke mmoja aliyesaidia kuandaa maandamano haya, Amina Cachalia.

https://p.dw.com/p/CHmo
Picha kutoka Afrika Kusini ya mwaka 1965: Wazungu walikaa kwenye benchi, Waafrika chini
Picha kutoka Afrika Kusini ya mwaka 1965: Wazungu walikaa kwenye benchi, Waafrika chiniPicha: AP

Leo miaka 50 iliyopita, ilikuwa siku nzuri sana, kama Amina Cachalia anavyokumbuka:

“Ilikuwa asubuhi ya baridi. Tulichukua miezi mitano kuandaa maandamano haya. Tulipita nyumba hadi nyumba. Tulizungumza na wafanyakazi wanawake wa viwandani. Tuliongea na wanawake mabarabarani au kwenye vituo vya basi ili kuwaeleza juu ya mpango wetu wa kufanya maandamano makubwa tarehe 9 Agosti na kutembea hadi ikulu. Tulimuomba kila mmoja ashiriki. Hatukujua wangapi watakuja, lakini walikuja kwa wingi. Ilikuwa maandamano wa amani na heshima.”

Lengo la maandamano lilikuwa kupinga sheria za pasiporti ambazo ziliwalazimisha wanawake wote wasiokuwa wazungu kubeba pasiporti kila pahala walipokwenda ili kuona iwapo wana haki ya kuwepo huko. Sheria hizo zilikuwa sehemu moja katika mfumo wa ubaguzi wa rangi uliogusa kila eneo la maisha.

Bibi Amina Cachalia anaeleza kwamba hadi kufikia umri wa miaka 18 alikuwa na maisha mazuri bila ya kujali rangi ya watu katika mtaa wake wa alikozaliwa, Newclare, mjini Johannesburg. Mwaka 1948 lakini serikali chini ya chama cha National Party, ilianzisha mfumo wa ubaguzi wa rangi unaojulikana kama Apartheid. Kuanzia hapo, Amina Cachalia alipinga serikali hiyo, na mara kwa mara alishikwa na polisi kwa kuvunja sheria za ubaguzi.

Anakumbuka: “Tumefungwa gerezani kwa wiki mbili na ulikuwa wakati mzuri. Kwa mara ya kwanza tuliweza kukaa pamoja, wanawake wa kila rangi. Huko nje tulitengwa.”

Vita dhida ya Apartheid viliwaunganisha wanawake wa Afrika Kusini. Licha ya maandamano ya tarehe 9 Agosti hayakuweza kuondosha sheria za pasiporti, hata hivyo yalikuwa na umuhimu wa kisiasa, kwani umoja wa wanawake ulipata nguvu. Mpaka leo wanawake walifanikiwa kwa kiwango kikubwa, anasema Bi Cachalia akitaja kuwa zaidi ya asimilia 30 ya wabunge ni wanawake na pia karibu nusu ya mawaziri ni wanawake.

Bado lakini wanawake wanakabiliwa na changamoto kubwa nchini Afrika Kusini. Bi Cachalia anasema: “Hadi sasa wanawake ni wahanga wa matumizi ya nguvu. Tatizo lingine ni maradhi ya ugonjwa wa ukimwi. Kila siku ninaomba wanawake wajiunganishe, wasaidiane na washauriane katika suala hilo. Wanaweza kupita nyumba hadi nyumba kama sisi tulivyofanya ili kuwaelimisha wanawake vijana kuhusu ukimwi.”