1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miaka 60 ya uhuru wa India

Oummilkheir14 Agosti 2007

India yasherehekea ufanisi wa kiuchumi miaka 60 baada ya uhuru,ingawa umaskini pia umekithiri

https://p.dw.com/p/CH9e
Kinu cha kinuklea cha Maadras nchini India
Kinu cha kinuklea cha Maadras nchini IndiaPicha: AP

Hatua za usalama zimeimarishwa tangu katika maeneo ya milimani ya Kashmir,kupitia misitu ya eneo la kati la India hadi katika miji inayotikiswa kwa matumizi ya nguvu kaskazini mashariki,ambako maelfu ya wanajeshi wanapiga doria kusimamia usalama wakati huu ambapo India nzima inasherehekea miaka 60 ya uhuru wake.

Hatua za usalama zimeimarishwa kufuatia onyo la mashambulio lililotolewa na magaidi wa Al Qaida na waasi wanaopigania kujitenga kwa jimbo la Kashmir,mnamo siku hii ya leo ya kuadhimisha miaka 60 ya uhuru nchini India.

Pekee katika mji mkuu New-Delhi,walinzi 70 elfu wa amani na wanajeshi wanapiga doria katika majengo ya serikali na mitaa kunakokutikana ofisi za mabalozi pamoja na kulinda usalama katika njia panda zote muhimu za jiji hilo lenye wakaazi milioni 14.

Kila mwaka,wakati wa kuadhimisha siku kuu ya uhuru,Agosti 15,viongozi wanaonya dhidi ya vitisho vya magaidi na kuimarisha usalama nchini.

“Jibu letu ili kujihifadhi ni lile lile,naiwe panapohusika na vitisho vya magaidi wa Al Qaida au kundi la wanaopigania kujitenga kwa jimbo la Kashmir-Lashkar-e Taiba” amesema mkuu wa idara ya usalama inayopambana na visa vya kigaidi miongoni mwa Polisi ya mjini New-Delhi,Samsher Deol.

“Hakuna jipya kuhusiana na Al Qaida,lakini tunajihadhari” ameongeza kusema.

Lakini katika kanda ya Video iliyotangazwa Agosti tano iliyopita,Al Qaida wametishia kuhujumu ofisi za ubalozi za nchi za magharibi kokote kule ziliko ulimwenguni-na hasa mjini New-Delhi.Katika kanda hiyo ya video,India imetuhumiwa “kuwauwa zaidi ya waislam laki moja huko Kashmir kwa ridhaa ya Marekani.”

Maeneo mengine ya mji mkuu yanayopakana na majimbo ya India yatafungwa pia hii leo na hakuna ndege yeyote itakayoruhusiwa kuruka katika anga ya New-Delhi.

Treni zinazomilikiwa na serikali-shabaha kubwa ya mashambulio ya kigaidi zinasachiwa moja hadi nyengine.

Hatua kali za ulinzi zimeimarishwa piaAssam,jimbo la kaskazini mashariki ya India na katika eneo la Kashmir .Mji mkuu Srinagar na uwanja wa michezo wa karibu na hapo vimefungwa pia kuepusha mashambulio yasitokee katika sherehe za miaka 60 ya uhuru.

Waasi wa Kashmir na wanamgambo wengineo wanaitaja siku ya uhuru wa India kua ni “siku ya kiza”-na mara nyingi wamekua wakifanya mashambulio kwa lengo la kufuja sherehe za uhuru.

Waziri mkuu wa India Manmohan Singh anatazamiwa kufungua sherehe za uhuru hii leo kutoka ngome kongwe ya karne ya 16- Mughal Red Fort ambayo imeshafungwa,hakuna yeyote anaeruhusiwa kuisogelea.Mizinga 21 itafuatia kabla ya waziri mkuu huyo kuhutubia taifa na kuchambua miaka 60 ya uhuru wa India.

Tangu uhuru Agostzi 15 mwaka 1947,India imepiga hatua kubwa mbele,ikijivunia nguvu za kinuklea na ukuaji imara wa kiuchumi pamoja na kung’ara katika jukwaa la kimataifa.

Wadadisi wa benki za kigeni wanaashiria India itashikilia nafasi ya tatu ya kiuchumi ulimwenguni mnamo mwaka 2025,mbele ya Japan.Ifikapo mwaka 2050 India inakadiriwa kuipita hata Marekani na kushikilia nafasi ya mwanzo ya kiuchumi ulimwenguni,sawa sawa na jamhuri ya umma wa china.

“Dunia iko chini yetu”liliandika kwa fakhari gazeti la Times of India,huku lile la Hindustan Times likiashiria “India ndio dola kuu la siku za mbele.”

Akihojiwa kuhusu mustakbal wa India waziri wa biashara Kamal Nath amesema tunanukuu:”India ndio Mustakbal.”

Licha ya yote hayo lakini nchi hiyo yenye wakaazi bilioni moja nukta moja inashika usukani pia miongoni mwa nchi ambako shida na ukosefu wa usawa umekithiri.

Kuna mamilioneya laki moja na watu wengine milioni 70 ambao mishahara yao inalingana na ile ya wafanyakazi wa nchi za magharibi.Lakini kati ya wafanyakazi milioni 457 wa nchi hiyo,asili mia 90 wanalipwa nusu dola kwa siku.Na asili mia 46 ya watoto wenye umri wa chini ya miaka mitatu hawapati chakula bora.

Idadi ya wasiojua kusoma na kuandika imegonga asili mia 60 na asili mia 78 hawana vyoo.