1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Michel Platini ndie rais mpya wa UEFA

Ramadhan Ali26 Januari 2007

Nahodha wa zamani wa timu ya Taifa ya Ufaransa,Michel Platini alichaguliwa leo huko Dusseldorf kuwa rais mpya wa UEFA-shirikisho la dimba la Ulaya.Alimshinda rais wa hadi sasa Mswede,Lennart Johanson.

https://p.dw.com/p/CHcl

Nahodha huyo wa zamani wa Le Blues-timu ya taifa ya Ufaransa na wa klabu ya Itali ya Juventus,amemuangusha alaasiri ya leo mzee Lennart Johansson wa Sweden aliekin’gan’gania kiti cha rais wa UEFA-shirikisho tajiri kabisa duniani la dimba kwa kipindi cha miaka 16.

Wapiga kura leo katika Hilton Hotel, mjini Dusseldorf,hapa Ujerumani, wamemwambia mzee Johansson „pumzika na siku zako zimekwisha-n’gatuka.“

Kutoka No.10,Michel Platini leo amebadili jazi na kuwa No.I.Platini leo hii ijumaa ametimiza ndoto yake ya kutaka nafasi ya kuliongoza na kulisarifu dimba la Ulaya nje ya chaki ya uwanja .Platini, ni mmoja kati ya mastadi wachache wa dimba barani humu mkuchaguliwa ‚Mwanasoka bora wa mwaka mara tatu“.

Sasa uwanja kwake ni wazi kwa stadi huyu wa miaka 51 kuanza kutekeleza ahadi alizozipa nchi changa za Ulaya sauti kubwa katika maamuzi ya UEFA-shirikisho lililodhibitiwa na dola kuu za dimba-Ujerumani,Uingereza,Itali na Spain.Beckenbauer,alieandaa kombe lililopita la dunia hapa Ujerumani, bila shaka, hakufurahia kuchaguliwa kwa Michel Platini,sawa na shirikisho la dimba la Ujerumani.Rais wa FIFA-Sepp Blatter,amekaribisha uchaguzi wa Platini aliemuita „rafiki yake wa chanda na pete“ tangu Platini alipoandaa Kombe la dunia 1998 lililomalizikia ushindi wa Ufaransa nyumbani.

Akiwa ni mwana wa mchonga mawe wa kitaliana kutoka Piedmont,Itali,Michel Platini alipata umaarufu kama ule wa nahodha wa karibuni wa timu ya Ufaransa -Zinedine Zedane.Alivaa jazi nambari 10 kuiongoza Ufaransa-jazi inayovaliwa na mastadi wale tu kama Pele na Maradona,Zedane na Platini-wachezaji waliojaaliwa ufundi wa kuwachezesha wenzao kutia magoli na ule wa wao binafsi kuona wavu.Pele,Maradona,Zedane na Platini walikua na sifa hizo.

Akishukuru kwa kuchaguliwa katika wadhifa war ais wa UEFA,Platini alisema:

„Hu uni mwanzo wa changamoto.Nataka kumshukuru kila mmoja alieonesha utiifu kwangu.Nina furaha kuweza kuliwakilisha kabumbu la ulaya.“

Mnamo miaka ya 1980 wakati akizichezea klabu za Nancy,St.etienne na Juventus, Platini alikuja kuchaguliwa „Mwanasoka bora wa mwaka wa Ulaya“ tena mara 3 mfululizo:1983,1984 na 1985.

1984 kama nahodha wa Ufaransa, Platini aliongoza timu yake kutwaa kombe la Ulaya la Mataifa nyumbani.Baada ya kustaafu ,kipindi chake cha miaka 4 kama kocha wa Ufaransa, hakufua dafu.1992 kwahivyo, Platini alijiuzulu baada ya Ufaransa kupigwa kumbo katika duru ya kwanza ya finali za kombe la Ulaya la mataifa.

Kabla Ufaransa kuandaa Kombe la dunia 1998 nyumbani,Platini alishirikiana na rais wa shirikisho la kabumbu la Ufaransa Fernand Sastre.Kwa pamoja walisimamia kampeni ilioongoza Ufaransa kutawazwa kwa mara ya kwanza mabingwa wa dunia na taji la pili tangu lile la Ulaya,1984.

Mwaka mmoja baadae, Platini aliamua kujitupa upande wa Sepp Blatter,rais wa FIFA na yeye akawa mshauri wake wa dimba.Alipoteuliwa makamo-rais wa shirikisho la dimba la Ufaransa 2001,Michel Platini, ndipo alipoanza kuparamia ngazi iliomfikisha pale alipo leo.2002 akawa mjumbe wa kamati-tendaji ya mashirikisho yote 2-UEFA la Ulaya na FIFA la dunia.

Matarajio ya kuchaguliwa kwa kipindi cha 5 kwa mpinzani wake-Lennart Johansson, kuliegemea mafanikio yake na hasa katika kuongoza champions –League.Platini ameahidi mageuzi makubwa katika mfumo huo.