Michezo: Kombe la vilabu bingwa ulaya-Champions league Jumanne
23 Oktoba 2007
Mabingwa wa Uhispania Barcelona wanaingia uwanjani kuchuana na Rangers ya Scotland baada ya kuanza michuano hiyo kwa kushinda michezo miwili. Kilabu hizo mbili hazijawahi kukutana na Rangers inajiwekea matumaini baada ya ushindi wa mabao 3-0 katika mechi ya ligi ya kukata na shoka Jumamosi iliopita nyumbani dhidi ya mahasimu wao Celtic. Barcelona lakini kwa mshangao ilifungwa kwa mara ya kwanza msimu huu iliadhibiawa mabao 3-1 na Villareal.
Rangers hawakufungwa katika mechi nane za Champions league, wakati Barcelona ina rekodi mbaya panapohusika na kuchuana na vilabu vya Scotland, ikiwa imewahi kushinda mechi mbili tu kati ya 12.
Kwa upande wa Manchester United ya England ambao Jumamosi iliopita waliibwaga Aston Villa katika mchezo wa ligi kuu Premier Leagie ukiwa ushindi wa tisa msimu huu, wanaelekea Kiev Ukraine kuvaana na Dynamo Kiev ambayo b imeshindwa michezo yake miwili katika kundi F na kucheza jumla ya mechi tisa za Champions League-ligi ya vilabu bingwa bila ya mafanikio.
Arsenal miamba wengine kutoka England wanaikaribisha Slavia Prague ya Jamhuri ya Cheki katika kundi H wakisaka ushindi wa 12 katika mashindano jumla. Hadi sasa Arsenal au Gunners kama wanavyofahamika nyumbani mjini London, hawakufungwa hata bao moja ikiwa ni pamoja na ushindi wa mabao 5-0 katika mechi zote mbili, wakati wa mzunguko wa kwanza walipoipa funzo Sparta, mahasimu wa nyumbani wa Slavia,
Kwengineko leo hii Stuttgart mabingwa wa Ujerumani wanamenyana na Olympique Lyon ya Ufaransa katika kundi E, As Roma inatoana jasho na Sporting Lisbon ya Ureno katika kundi F , Kundi G ni CSKA Moscow ya Urusi inatoa jasho na Inter Milan ya Itali , huku mechi nyengine ya kundi hilo ikiwa ni ile ya kati ya PSV Eindhoven ya Uholanzi ikiikaribisha Fenerbahce ya Uturuki na kundi la H ni mchuano kati ya Sevilla ya uhispania dhidi ya Steua Bucharest ya Rumania.
Baada ya michezo ya leo, miongoni mwa mechi za kesho ni pamoja na Real Madrid itakayoumana na Olympiakos ya Ugiriki. Madrid chini ya Kocha mjerumani aliyewahi pia kulisakata gozi katika kilabu hiyo Bernd Schuster imekumbwa na majeruhi msimu huu. Schuster alipewa hatamu baada ya mtaliani Fabio Capello, akiahidi ushindi na soka la kuwavutia mashabiki wake.