1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Michezo mwishoni mwa wiki, Bayern Munich yapambana na Leverkusen

Oumilkher Hamidou9 Aprili 2010

Mara tu baada ya kurejea kutoka shimo la tewa huko Manchester, salama usalimini, Bayern Munich, ina miadi leo na Bayer Leverkusen kunyang´anyia pointi 3 zinazoweza kuamua taji la bundesliga msimu huu linaenda wapi

https://p.dw.com/p/MsAH
Bayern Munich yashangiriaPicha: AP

Katika Premier League, Liverpool na Fulham, zimefuta aibu ya timu za Uingereza-Manu na Arsenal, katika champions league msimu huu kwa kufuzu kuingia nusu-finali ya Kombe la Ligi la ulaya-zamani UEFA Cup.

Kocha wa Manchester United Sir Alex Ferguson,ameitaka timu yake kutamba kesho mbele ya Blackburn, ili kufuta madhambi hayo na kuparamia kesho kileleni mwa Premier League.

Kikosi cha Louis van Gaal,kimeazimia kutoroka na vikombe 3 msimu huu:Champions League,Kombe la Taifa la Ujerumani na Taji la Bundesliga:Ili kuitimiza shabaha hiyo ,Munich lazima itambe leo nyumbani mwa Bayer Leverkusen na kuondoka na pointi zote 3. Leverkusen, iliongoza Ligi hii mapambano 24 bila kushindwa , sasa imeteleza hadi nafasi ya 3 ya ngazi ya Ligi na ikicheza nyumbani leo,haingependa kutoa sadaka zaidi kwa Munich.

Bayern Munich, inaongoza Bundesliga, wakati huu kwa pointi 1 mbele ya Schalke.Schalke, mwishoni mwa wiki hii, inapambana na Hannover iliomo hatarini kuteremshwa daraja ya pili.Hivyo, Schalke, ina kibarua kigumu kuigaragaza chini Hannover itayovinjari isikate roho.

Timu iliopo mkiani mwa Ligi kutoka jiji kuu Berlin, inatumai kuendeleza vishindo vyake vya karibuni vilivyoipatia jumla ya pointi 6 kutoka mapambano 2.Wanabidi Stuttgart .Mainz leo, inachuana na Borussia Moenchengladbach wakati Hoffenheim inaikaribisha FC Cologne.Cologne haimudu pigo jengine leo baada ya lile la nyumbani walilopewa na Berlin.Werder Bremen, inacheza na Freiburg.

Kesho, Bochum, inahetimisha kalenda ya dimba la mwishoni mwa wiki hii kati yake na Hamburg, iliotamba mbele ya Liege ya Ubelgiji hapo juzi na kufuzu kwa nusu-finali ya Ligi ya ulaya.Mabingwa Wolfsburg, waliotimuliwa nje ya Kombe hilo na Fullham ya Uingereza, ni wageni wa Nüremberg huko kusini mwa Ujerumani.

Ama katika Premier League,Sir Alex Ferguson ,ameamua kutotoka mikono mitupu msimu huu bila ya kombe.Mara tu baada ya vishindo vya Manu vya mabao 3 katika lango la Bayern Munich, kubainishiwa hayatoshi kubakia champions league, ameamrisha timu yake kuiadhibu kesho Blackburn kana kwamba, ni Blackburn iliowasababishia msiba wa juzi Jumatano usiku.

Chelsea, ikiwa na miadi na Aston Villa katika nusu-finali ya kombe la FA leo, Manu, inaweza kesho kuparamia tena kileleni mwa Premier League kwa kuitimua nje Blackburn.Hatahivyo, Manu itabidi kuteremka kesho bila ya mzinga wao uliotetereka-Wayne Rooney.Na mara hii, hakuna kudanganya kama walipocheza juzi na Bayern Munich. Ingawa Kombe la Ligi halina hofu kwa Manu, pigo alilowapa muaivory Coast Didier Drogba, Jumamosi iliopita, limewashikisha adabu na kuwatia moyo Chelsea, kuamini kwamba ,huu ni msimu wao wa kukimbia London na taji la Premier League.

Hull City, inaikirimu nyumbani Burnley katika changamoto ya timu 2 za mkiani.West ham, inapapurana na Sunderland.Manchester City, yaweza kukaza kamba na kun'gan'gania nafasi ya 4 ya ngazi ya Premier League mradi tu kesho, ingurume kamba simba mbele ya Birmingham,siku ambayo Liverpool mara tu baada ya kufuzu kwa duru ijayo ya Kombe la Ligi la ulaya, inaikaribisha Fulham, iliowakongoa meno mabingwa wa Ujerumani, Wolfsburg na kuwaacha vibogoyo nje ya Kombe hilo.

Mwandishi: Ramadhan Ali /AFPE

Uhariri: Sekione Kitojo.