Miji iliyotelekezwa Sudan Kusini
20 Januari 2014Mbunge wa zamani Reath Muoch Tang anamuonyesha mmoja wa vijana akiwa amelala katika dimbwi la damu, kichwa chake kikiwa kimepasuliwa kwa risasi. "Huyu ni kaka yangu mkubwa. Watu wenye silaha walio karibu na rais Salva Kiir walimuua Desemba 17," anasema wakati akionyesha picha ya marehemu katika simu yake aina ya Smart Phone.
Chale zinazoonekana usoni mwa Tang zinamtambulisha kama Mnuer na kwa hivyo muasi ambaye anamuunga mkono makamu wa zamani wa rais Riek Machar. Tang alifanikiwa kuikimbia nchi yake mapema, na amejiunga na ujumbe wa waasi wa Machar, ambao kwa sasa unajadili usitishaji wa mapigano mjini Addis Ababa na upande wa serikali, unatawaliwa na kabila hasimu la Dinka.
Anasema maadamu Kiir bado yuko madarakani, hawezi kurudi tena nyumbani kwa sababu watamuuwa mara moja. Tangu katikati mwa mwezi Desemba, maisha ya kila siku yamegeuka kuwa uwanja wa kivita kwa maelfu ya raia wa Sudan Kusini.
Ni miji iliyotelekezwa
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anaeshughulikia haki za binaadamu Ivan Simonovic ameyatembela majimbo yaliyomo katika mapigano katika siku chache zilizopita kwa lengo la kujionea mwenyewe hali halisi. Simonovic ameitembelea miji ya Bor na Bentiu, miji mikuu ya majimbo yenye utajiri mkubwa wa mafuta, ambako waasi na wanajeshi wa serikali wanapigana kuyadhibiti.
Naibu Katibu Mkuu huyo ameulezea mji wa Bor kama mji uliyotelekezwa kabisaa, usiyo na uhai wala watu. Anasema ili kuona watu, unapaswa kwenda kambini. Huko Bentiu ndiyo usiseme kabisaa, anasema Simonovic, na kuongeza kuwa mji huo kwa sasa ni kama haupo tena kutokana na kuchomwa kabisaa.
Tayari asilimia kubwa ya wakaazi wa nchi hiyo walikuwa wanaishi katika hali ya umaskini kabla hata ya kuanza kwa mapigano. Theluthi tatu wanaendelea kuwa wajinga. Lakini kabla ya vita jitihada za kujenga miundombinu inayohitajika kwa ajili ya ukuaji wa kiuchumi zilikuwa zinaendelea, na wawekezaji walikuwa wanaanza kuonyesha nia.
Lakini hayo yote sasa yamekwisha. Raia wengi wa kigeni walikibizwa katika maeneo salama wiki kadhaa zilizopita, na ni wachache tu walio na uwezekano wa kurudi. Wakati huo huo, zaidi ya laki nne miongoni mwa wenyeji wamepoteza kila kitu - makaazi yao, mifugo yao, na njia za kujikimu kimaisha.
Utegemezi zaidi wa misaada
Badala ya ukuaji wa kiuchumi, Sudan Kusini sasa inategemea misaada kwa kiasi kikubwa. Lakini hata hii ama inazuwiwa kuyafikia maeneo ambako inahitajika zaidi, au inaporwa njiani. Shirika la Madaktari wasio na mipaka MSF, limelaazimika kusitisha shughuli zake katika mji wa kaskazini wa Malakal katika jimbo la Upper Nile, ambako lilikuwa likitoa huduma muhimu, na kuna matarajio madogo sana kwao kuanzisha tena utoaji wa huduma hizo.
Mkurugenzi mkuu wa MSF Arjan Hehenkamp, alisema kuwa watu wenye silaha waliingia katika ofisi za shirika hilo mara mbili wakapora na kuwatishia wafanyakazi, na kwamba shirika halikuwa na njia nyingine isipokuwa kusimamisha shughuli zake katika hospitali ya Malakal.
Safari ndefu ya kusitisha uhasama
Kusitishwa kwa mapigano ndiyo kipaumbele cha kwanza cha wanadiplomasia wa kimataifa na maafisa wa misaada, lakini pande hasimu zinaonekana kwa sasa haziko tayari kufanya hata tahfifu katika mazungumzo yanayofanyika katika hotel ya kifahari mjini Addis Ababa Ethiopia, licha ya fununu za kufikiwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano hayo mwishoni mwa wiki.
Waangalizi wanaona kama majadiliano hayo yametawaliwa na hisia za kila upande kujiona ndiyo bora, uroho wa madaraka na utiifu kwa makabila yao, wakati nchi nzima ikitumbukia katika machafuko na uharibifu.
Mwanadishi: Iddi Ismail Ssessanga/dpae
Mhariri: Mohamed Abudl-Rahman