1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miripuko yazidi kuitikisa Urusi

Abdu Said Mtullya30 Desemba 2013

Watu wasiopungua 10 wameuawa katika shambulio lingine katika mji wa Volgograd kusini mwa Urusi. Siku ya Jumapili watu 17 waliuawa baada ya mshambuliaji wa kujitoa mhanga kujiripua kwenye stesheni ya treni.

https://p.dw.com/p/1AiTy
Shambulio la Jumatatu dhidi ya Basi mjini Volgograd liliwauwa watu wasiopungua 10.
Shambulio la Jumatatu dhidi ya Basi mjini Volgograd liliwauwa watu wasiopungua 10.Picha: Reuters

Shambulio la Jumatatu litawafanya watu wawe na hofu kubwa zaidi juu ya hali ya usalama wakati wa mashindano ya michezo ya olimpiki ya kipindi cha baridi inayotarajiwa kuanza tarehe saba mwezi Februari katika mji wa burudani wa Sochi uliopo umbali wa kilometa 690 kusini magharibi ya mji wa Volgograd.

Russland Wolgograd Explosion Anschlag Bus 30. Dez. 2013
Basi la abiria likiwa limeshambulia mjini Volgograd.Picha: Reuters

Bomu lililotumika katika shambulio la leo lililiteketeza kabisa behewa la treni ya barabarani ambalo lilikuwa limejaa abiria. Kwa mujibu wa taarifa ya televisheni madirisha ya nyumba za karibu pia yaling'oka kutokana na nguvu ya bomu.

Kamati ya uchunguzi ya Urusi imesema maafisa wa usalama wameanza kufanya uchunguzi juu ya shambulio hilo linalotuhumiwa kuwa ni kazi ya magaidi. Shambulio la hapo Jumapili pia lilifanyika kwa bomu lililokuwa na nguvu kubwa.

Mfumo wa usalama uliepusha maafa makubwa
"Kulingana na uchunguzi wa awali, nguvu ya bomu hilo ilikuwa sawa na kilo kumi za baruti. Na hakika watu wengi zaidi wangelikufa laiti mfumo wa kwenye kituo cha treni usingelifanya kazi," anasema afisa wa idara ya uchunguzi Wladimir Markin.

Kutokana na mfumo huo wa usalama kufanya kazi, mshambuliaji wa kujitoa mhanga hakuweza kuingia katika ukumbi wa abiria ambako watu wengi walikuwa wanasubiri. Kamati ya kitaifa kupambana na ugaidi ya nchini Urusi imesema shambulio la Jumatatu tofauti la Jumapili, yumkini lilifanyika kwa bomu lililotegwa kati kati ya behewa la tramu, badala ya kufanywa na mshambuliaji wa kujitoa mhanga.

Lakini shirika la habari la Itar -tass limeambiwa na chanzo kimoja kwamba yumkini shambulio la Jumatatu lilifanywa na mwanamume aliejitoa mhanga. Jumapili alikuwa mwanamke aliejiripua.

Idara kuu ya usalama ya Urusi imeshawasilisha taarifa kwa Rais Vladimir Putin juu ya kadhia ya Jumatatu.Televisheni ya taifa imeripoti kwamba watu sasa wanakwepa kutumia mabasi na treni za barabarani kutokana na shambulio la Jumapili katika mji wa Volgograd.

Kituo cha treni cha mjini Volgograd kilichoshambuliwa siku ya Jumapili.
Kituo cha treni cha mjini Volgograd kilichoshambuliwa siku ya Jumapili.Picha: picture-alliance/dpa

Uvumi juu ya mashambulizi zaidi
Wakati huo huo uvumi umeenea katika mitandao ya kijamii kwamba pamekuwapo na mashambulio zaidi lakini idara husika zimekanusha.Uchunguzi unaofanywa utaekelezwa hasa katika jimbo la Kaukasus lenye waislamu ambako waislamu wenye itikadi kali wamekuwa wanapambana na majeshi ya usalama ya Urusi kwa miaka mingi.

Kiongozi wa wapiganaji wanaotaka kuleta utawala wa kiislamu, katika jimbo lote la Kaukasus ya kaskazini Doku Omaror amewapa amri waasi ya kuwashambulia raia nje ya jimbo hilo na kuivuruga michezo ya Olimpiki ya kipindi cha baridi inayotarajiwa kufanyika katika mji wa burudani wa Sochi.

Mwandishi:Mtullya Abdu/afp,rtre.
Mhariri:Daniel Gakuba