1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa ataka kuundwa serikali haraka DRC

25 Julai 2019

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Leila Zerrougui amemtaka rais wa sasa na wa zamani wa nchi hiyo kukubaliana haraka hatua ya kuunda serikali mpya

https://p.dw.com/p/3MhoK
Demokratische Republik Kongo | Félix Tshisekedi | Provinzparlament Upper Katanga
Picha: Presidence RDC/G. Kusema

Akizungumza jana katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Zerrougui amesema kuwa mazungumzo mazito yanaendelea kati ya chama cha Rais Felix Tshisekedi na muungano wa vyama vinavyomuunga mkono rais wa zamani wa Kongo Joseph Kabila. Mjumbe huyo wa Umoja wa Mataifa ameonya kuwa kucheleweshwa kwa jambo hilo kwa miezi miwili kunaathiri kipindi cha mpito nchini humo.

Zerrougui ameelezea wasiwasi wake kuhusu hali ya kisiasa nchini Kongo, akisema kukosekana kwa serikali inayofanya kazi, kunakwamisha kuanzisha uhusiano na washirika pamoja na kutekeleza mageuzi muhimu ambayo Tshisekedi aliyaahidi. Ameliambia baraza hilo la usalama kwamba vurugu katika maeneo yenye mizozo bado zinaleta athari kubwa kwa raia na kwamba mapigano bado yanaendelea kwenye maeneo kadhaa ya Kongo hasa mashariki mwa nchi hiyo.

Mjumbe huyo wa Umoja wa Mataifa amesema katika miezi ya hivi karibuni amewahimiza wachangiaji muhimu wa kisiasa kulinda faida zilizopatikana wakati wa uchaguzi na kipindi cha amani cha mpito na kuhakikisha wanaunda serikali. Katika mwelekeo ulio mzuri, Zerrougui amesema Tshisekedi amesema anakusudia kuanzisha mageuzi ambayo kama yatatelekezwa, yanapaswa kuimarisha taasisi za serikali na kuboresha maisha ya watu wa Kongo.

Umoja wa Mataifa unatambua juhudi za Kongo kudumisha mahusiano na nchi jirani

Zerrougui amebainisha kuwa Umoja wa Mataifa pia umeona maendeleo kwenye hatua zilizopigwa kama vile kuimarika uhusiano kati ya Kongo na majirani zake, tangu Tshisekedi alipoingia madarakani. Amefafanua kuwa kiongozi huyo wa Kongo amedhamiria kuufanya ukanda wa Maziwa Makuu kuwa eneo salama, lenye amani na maendeleo.

Leila Zerrougui
Mjumbe maalumu wa Umoja wa mataifa Leila ZerrouguiPicha: picture-alliance/epa/M. Trezzini

Tshisekedi alitangazwa mshindi katika na kuchukua nafasi ya Kabila aliyeiongoza Kongo kwa miaka 18. Hata hivyo, ushindi wa Tshisekedi ulipingwa na mgombe wa upinzani, Martin Fayulu ambaye ameendelea kushikilia msimamo wake kwamba alishinda urais katika uchaguzi huo, ingawa alishindwa katika rufaa yake.

Huku Tshisekedi akishikilia nafasi ya urais, muungano wa vyama vinavyomuunga mkono Kabila ulishinda kwa wingi katika uchaguzi wa bunge uliofanyika mwezi Januari. Hata hivyo, Tshisekedi alilazimika kuweka mpango wa kugawana madaraka ili kuepusha mvutano kati yake na vuguvugu la mtangulizi wake, akimuweka Sylvestre Ilunga kuwa Waziri Mkuu anayeratibu mazungumzo na chama chake.