Mjumbe wa UN nchini Libya ajiuzulu huku akiwalaumu wanasiasa
17 Aprili 2024Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Libya Abdoulaye Bathily amesema amewasilisha ombi la kujiuzulu, akisema shirika hilo la kimataifa haliwezi kufanikiwa kuunga mkono mabadiliko ya kisiasa ya nchi hiyokwa sababu viongozi wake wameyaweka maslahi yao mbele badala ya kutafuta suluhisho.
Soma pia:Makazi ya waziri mkuu wa Libya yashambuliwa
Bathily ambaye ni raia wa Senegal ameyasema hayo katika kikao na waandishi habari baada ya mkutano wa Baraza la Usalama ambapo alielezea hali ilivyo mbaya katika nchi hiyo ya Afrika Kaskazini, iliyokumbwa na mzozo na vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa zaidi ya muongo mmoja.
Bathily amesema Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya - UNSMIL ulifanya juhudi nyingi chini ya uongozi wake katika kipindi cha miezi 18 iliyopita lakini hali imekuwa mbaya zaidi kutokana na ukosefu wa dhamira ya kisiasa na nia njema kutoka kwa viongozi wa Libya. Ameiita hali hiyo kuwa ya kuhuzunisha kwa sababu idadi kubwa ya watu wa Libya wanataka kuondoka katika fujo hiyo.