1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkataba wa kupunguza silaha za nuklia

Nina Markgraf7 Aprili 2010

Rais Obama na Medwedev watia saini leo Prague

https://p.dw.com/p/MpX9
Barack ObamaPicha: AP

Nia hasa ya rais Barack Obama , katika kutia saini Mkataba wa kupunguza makombora ya nuklia yanayovuka bara moja hadi jengine (START) kwa ufupi, mjini Prague, hii leo, ni kuzuwia kutapakaa kwa silaha za kinuklia.Ni mjini Prague, Jamhuri ya Czech ambako Rais Obama , kwa mara ya kwanza alichambua mtazamo wake wa a dunia bila ya silaha za nuklia.Na ni katika mji huo leo, atatia saini mkataba wenye shabaha hiyo pamoja na rais Medvedev wa Urusi.

Makubaliano ya kutia saini Mkataba mpya wa kupunguza silaha za kinuklia walilifikia marais hao wawili wa Marekani na Urusi katika mazungumzo yao ya simu mwishoni mwa mwezi uliopita wa Machi.Idadi ya vichwa vya makombora ya kinuklia, vitapunguzwa kila upande kutoka kima cha 2,200 hadi 1550.Idadi ya makombora yanayopakia vichwa hivyo, yatapunguzwa kwa nusu na kila upande kwa kima cha 800.Rais Obama ameyaeleza makubaliano hayo kati ya urusi na marekani kuwa ni mkataba muhimu sana wa kupunguza silaha tangu miongo 2 iliopita:

"Tunaimarisha juhudi zetu ulimwenguni kuzuwia kuzagaa kwa silaha hizi.Tunayatia shime mataifa mengine kutekeleza nayo wajibu wao katika swali hili."

Wayne Merry, wa baraza la maswali ya nje mjini washington anasema kuwa, Rais Obama anazungumzia zaidi kutoenezwa silaha za nuklia:"Kwa Utawala huu,hamu yake zaidi ni kutoenezwa silaha za nuklia kuliko kudhibiti silaha za Urusi."

Ingawa Wamarekani wanafunga Mkataba wa kupunguza silaha na Urusi, shabaha yao hasa ni Iran.Azma ni kufanya hali kuwa ngumu kwa Iran kuunda silaha zake za nuklia.Kwahivyo, Marekani na Urusi, kwanza zinajaribu kupiga mfano mwema na kupunguza maboma yao ya silaha.Halafu Marekani , inaandaa na kushiriki miezi ijayo msururu wa mikutano ya kimataifa juu ya mada ya usalama wa zana za nuklia -alao hivyo ndivyo asemavyo Wayne Merry:

Anaongeza kusema kwamba, kwa mkataba huu ,rais Obama anapiga ndege 2 kwa jiwe moja: Kwanza, anafungua ukurasa mpya katika usuhuba wake na Urusi.Na pili, anataka kwa ushirikiano na mataifa mengine kushiriki kwenye mkutano wa usalama wa silaha za nuklia April au katika mkutano wa kutoeneza silaha za nuklia mwezi Mei na kushinikiza shabaha hizo mbele ya Baraza la Usalama la UM.Baraza hilo litatakiwa kuiwekea vikwazo Iran ili ikomeshe mradi wake wa ujenzi wa silaha za nuklia.

Mkataba huu unaoitiwa saini leo mjini Pargue, utadumu miaka 10 na unashika nafasi ya ule wa START 2, uliomalizika muda wake Desemba mwaka jana.Mkataba huu utaanza kazi tu ukiidhinishwa pia na Baraza la Senate la Marekani.Na hatua hiyo, kutokana na mivutano ya siasa za ndani, inadhihirika ni shida.Kwani, ili kujipatia wingi wa thuluthi-mbili , itawapasa hata wabunge wa chama cha Republican kumuungamkono rais Obama.

Mwandishi: Soric,Miodrag/ DWashington.

Mtayarishi. Ramadhan Ali

Uhariri:Abdul-Rahman