Mkesha wa Krismas Bethlehem
24 Desemba 2010Huko Bethelem alikozaliwa Yesu Masia, maelfu ya watu kutoka kote duniani wamekuwa wakimiminika, wakiwemo kwa mara ya kwanza wakristo kutoka mataifa ya kiarabu yasiyokuwa na uhusiano wa kidiplomasia na Israel.
Tokea mapema leo asubuhi, mitaa ya mji huo wa Bethlehem uliyoko katika ukingo wa magharibi, imepambwa kwa miti na taa za Krismas.
Vijana wa kipalestina wakiwa wamevaa nguo za rangi ya bluu isiyo kooza wanajiandaa kwa mkesha huo, huku bendi ikifanya mazoezi na nyimbo za Krismas zikisikika kutoka katika maduka.
Polisi wa Mamlaka ya kipalestina wako imara kulinda usalama kuelekea katika eneo la Manger Syuare ambako kuna makanisa mawili lile la Nativity na la mtakatifu Catherine.Huko ndiko mkesha wa Krismas utakapofanyika.
Askofu wa Katoliki wa Mashariki ya Kati Latin Patriarch Fuad Twal ndiye atakayeongoza misa ya mkesha huo.
Atatoa ujumbe wa matumaini ya amani, lakini pia ataelezea masikitiko yake kuhusiana na mauaji ya waumini wa kikristo katika kanisa moja mjini Baghdad.Wakristo nchini Iraq wamekuwa wakishambuliwa mara kwa mara.
Kwa mujibu wa Mamlaka ya Palestina kiasi cha watu elfu 90 wanatarajiwa kushiriki katika mkesha huo wa Krismas.
Mwandishi:Aboubakary Liongo/AFP
Mhariri:Abdul Mtullya