Mkutano mkuu wa UEFA Dusseldorf
25 Januari 2007Kileleni mwa ajenda zake, ni kumchagua ama rais wa sasa Lennart Johansson kutoka Sweden abakie madarakani kwa kipindi cha miaka 4 zaidi na kileleni mwa UEFA au kumchagua rais mpya na kijana kwa miaka 26,mfaransa Michel Platini.
Michel Platini wa Ufaransa na Franz Beckenbauer wa Ujerumani-wawili kati ya mastadi wakubwa wa dimba barani Ulaya ,waweza kuchaguliwa kushika nyadhifa za juu kabisa katika mkutano mkuu wa UEFA-shirika la dimba barani ulaya.
Wakati Beckenbauer, mwenye umri wa miaka 61 aliiongoza Ujerumani kutwaa Kombe la Dunia la FIFA 1974 nyumbani na kama kocha 1990 huko Itali, Platini alikuwa nahodha wa Ufaransa na kuiongoza kutwaa Kombe la Ulaya la mataifa 1984.
Platini sasa ana umri wa miaka 51 wakati hasimu yake leo mzee Johansson ana umri wa miaka 77.
Ikiwa Platini atashindwa leo kufuata nyayo za mfaransa - rais wa kwanza wa FIFA, Jules Rimet,ambae Kombe la kwanza la dunia liliitwa kwa jina lake,Platini, hatakua na shughuli yoyote na UEFA kwa sasa.Kwani, hana dhamiri ya kugombea kuchaguliwa tena katika Halmashauri-tendaji ya UEFA baada ya kumaliza kipindi chake cha miaka 4 katika halmashauri hiyo.
Hatahivyo, Platini atasalia kuwa mjumbe katika Halmashauri kuu-tendaji ya FIFA-shirikisho la dimba ulimwenguni na hii alaokwa kipindi cha miaka 2 mingine.Kwahivyo, yamkini akatumika pamoja na Franz Beckenbauer,aliekuwa mwenyekiti wa Kamati ya Maandalio ya Kombe lililopita la dunia na ambae amearifu azma yake ni kusaidia kulinyanyua kabumbu barani Afrika.
Wakati kura ya kumchagua rais wa UEFA ndio ajenda ya usoni kabisa,uchaguzi pia unafanyika kwa viti 6 vilivyobakia vitupu katika Halmashauri-tendaji na wajumbe watawapigia pia kura kuwachagua wajumbe 3 wa UEFA kuiwakilisha katika Halmashauri kuu ya FIFA.
Kwani, David Will wa Scotland, anastaafu kama makamo-rais wa FIFA akiziwakilisha jumuiya 4 za mpira za Uingereza na nafasi yake itaamuliwa na jumuiya hizo 4 za Uingereza hapo Februari 5.
Mkutano wa leo (ijumaa) utajadili pia mageuzi kadhaa yanayopendekezwa kufanywa katika sheria za UEFA na mkutano unatarajiwa pia, kuidhinisha pendekezo kutoka chama cha mpira cha Scotland ‘scottish FA’, kuanzisha uchunguzi wa kupanua zaidi finali za Kombe la klabu bingwa barani Ulaya-champions League kutoka finali kwa timu 16 na kufanya 24.
Kikao cha Dusseldorf, kinapanga pia kuipatia uwanachama Jamhuri ya Montenegro iliojitenga mwaka jana na Serbia na kuwa mwanachama wake wa 53.Montenegro ilishiriki mwaka jana katika kombe la dunia kwa mara ya mwisho kama sehemu ya Serbia na Montenegro.Uanachama wa Gibralter, yamkini ukatiwa munda na hasa na Spain.
Macho kwahivyo, yanakodolewa Dusseldorf,Ujerumani,miezi 6 tu tangu firimbi ya mwisho kulia na kuitawaza Itali,mabingwa wa Kombe la FIFA la dunia.