1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa AU kutawaliwa na Sudan Kusini

Lilian Mtono15 Julai 2016

Hoja ya machafuko yanayoendelea kushika kasi nchini Sudan Kusini inatarajiwa kutawala katika mkutano unaowakutanisha viongozi wakuu wa Umoja wa Afrika, AU utakaofanyika Kigali, Rwanda.

https://p.dw.com/p/1JPO6
Südsudan Juba SPLA Rebellen
Picha: Getty Images/AFP/S. Bol

Sudan Kusini ni miongoni mwa majanga yanayotikisa bara la Afrika, ambalo viongozi hao watahitaji kulikabili, wakati ambapo pia kuna mgawanyiko kuhusu kiongozi atakayefaa kuongoza Umoja huo katika miaka minne ijayo.

Umoja wa Mataifa umeonya kuhusiana na hali ya wasiwasi na uwezekano wa kuzuka kwa mapigano mapya katika eneo la Juba, ambako kumekuwepo na utekelezwaji wa hatua ya kusitisha mapigano tangu jumatatu hii.

Lengo la Umoja wa Afrika la kuhakikisha amani inarejea kwenye bara lake ifikapo mwaka 2020, limepata pigo kufuatia machafuko hayo yaliyodumu kwa siku nne katika mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba na kusababisha vifo vya mamia na wengine 40,000 kuyakimbia makazi yao.

Machafuko haya ya hivi karibuni yamefuatia vita vya wenyewe kwa wenyewe, hali inayoelezwa kuvunjwa kwa makubaliano yaliyofikiwa mwaka jana ya kumaliza vita, iliyoanza baada ya rais Salva Kiir kumtuhumu kiongozi wa zamani wa waasi,ambaye sasa ni makamu wake, Rieck Machar kwa kuratibu mapinduzi.

Mwenyekiti wa AU anayemaliza muda wake, Nkosazana Dlamini-Zuma
Mwenyekiti wa AU anayemaliza muda wake, Nkosazana Dlamini-ZumaPicha: picture-alliance/dpa/ Y.Valat

"Kilichotokea Sudan Kusini hakikubaliki kabisa" amesema mwenyekiti wa Umoja wa Afrika anayemaliza muda wake, Dlamini Nkosazana Zuma, jumatano hii. Viongozi wa Sudan Kusini wanatakiwa kuwalinda watu wao, na si kuwa sababu ya mateso yao, aliongeza.

Mapema Jumatano hii, Rais Salva Kiir ameeleza nia yake ya kufanya mazungumzo na makamu wake baada ya kusitisha mapigano, ingawa anadai kuwa haikuwa rahisi kwa Rieck Machar kukubali mwito huo.

Tayari baadhi ya nchi zimeanza kuwaondoa raia wao nchini humo. Raia 156 wa India wamerejea nchini kwao. Ndege ya kwanza ya kijeshi iliwabeba raia wao mapema leo hii. Raia wengine walioondoka ni wa kutoka Nepal.

Hata hivyo hatua za kurejesha amani nchini Sudan Kusini zinaweza kukabiliwa na changamoto zaidi, kutokana na magawanyiko kuhusiana na mjadala wa kiongozi atakayefaa kupokea kijiti cha Dlamini-Zuma, na kuwa mwenyekiti mpya wa Umoja wa Afrika. Baadhi ya nchi zimesema hazitaunga mkono kiongozi yoyote kwa kuwa hakuna mwenye vigezo vinavyokubalika.

Majina matatu yanayotajwa katika kinyang'anyiro hicho ya Waziri wa mambo ya nje wa Botswana, Pelonomi Venson-Maitoi, mpinzani wake, kutoka Guinnea Agapito Mba Mokuy na makamu wa rais wa Uganda, Specioza Wandira-Kazibwe, yanahofiwa kushindwa kupata kura za kutosha kutoka katika Umoja huo wenye wanachama 54.

Baadhi ya nchi zimeanza kuwaondoa raia wao nchini Sudan Kusini
Baadhi ya nchi zimeanza kuwaondoa raia wao nchini Sudan KusiniPicha: picture alliance/AP Photo/Bundeswehr

Iwapo hilo litatokea, uchaguzi huo utaahirishwa na kufanyika upya katika mkutano ujao mjini Addis Ababa Ethiopia, Januari 2017.

Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa wa Afrika ya Kati, Abdoulaye Bathily amekuwa akijadiliwa kama mbadala, kama ilivyo kwa aliyekuwa rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete.

"Kamisheni iko tayari kufanya uchaguzi. Ipo minong'ono, lakini ni juu ya viongozi wa nchi kuamua kama wanataka kufanya uchaguzi ama la" amesema msemaji wa kamisheni ya Umoja huo Jacob Enoh Eben.

Mwandishi: Lilian Mtono/AFP/PTI.
Mhariri: Iddi Ssessanga