Mkutano wa kilele kati ya Umoja wa Ulaya na Afrika Abidjan
28 Novemba 2017Tayari mwishoni mwa wiki kansela Angela Merkel alisisitiza, aliposema kuimarishwa nafasi za masomo kwaajili ya vijana barani Afrika ni sehemu ya sera za maendeleo zilizolengwa kupambana na vyanzo vya ukimbizi.
Kwa maoni ya Angela Merkel na pia Umoja wa ulaya, uhusiano pamoja na Afrika utajipatia umuhimu mkubwa miongo inayokuja kuliko hata uhusiano pamoja na Marekani.
Hofu za wanaokimbilia kwetu kwaajili ya mizozo,zinatuhusu pia
Kabla hajaondoka kuelekea Abidjan waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujeumani Sigmar Gabariel , amesifu mchango wa Umoja wa Ulaya barani Afrika na kusema tunanukuu:" watu wanapokimbilia katika bara letu kwasababu ya kuhofia mizozo, hali hiyo inatuhusu na sisi pia huku Ulaya.Tukitaka kuzuwia mizozo, kusaidia kumaliza mivutano na kuhimiza amani basi tunahitaji kuhakikisha uwiano baina ya mkakati wa kisiasa, usalama , utawala bora na maendeleo."Amesema waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Sigmar Gabriel.
Kwa ushirikiano pamoja na washirika wa kimataifa, Ujerumani inataka kuhimiza ipatikane amani na usalama barani Afrika, inataka kusaidia mkakati wa Afrika wa kuimarisha amani na usalama na kusaidia kuimarisha juhudi za nchi za Afrika za kuepusha mivutano, kuipatia ufumbuzi mizozo inapotokea na kuimarisha utulivu.
Gerd Müller atawasaidia vijana wanaorejeshwa nyumbani baada ya kukataliwa kinga ya ukimbizi Ujerumani
Waziri mwenzake wa misaada ya maendeleo Gerd Müller ameserma kupitia kituo cha televisheni cha ARD anataka kuanzisha mpango wa kuwasaidia vijana wa Afrika waliokataliwa kinga ya ukimbizi humu nchini, kuanza maisha mepya nchini mwao.
Katika mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya na Afrika, unaoanza kesho mjini Abidjan nchini Côte d'Ivoire, kansela Merkel atazungumzia mpango wa mafunzo ya kazi kwa vijana utakaosimamiwa na Ujerumani, amesema waziri wa misaada ya maendeleo Gerd Müller.
Nayo jumuia inayosimamia jamii za watu wanaotishiwa maisha yao, imeutolea wito Umoja wa ulaya ijumuishe katika ajenda yao mapambano dhidi ya utumwa na uhalifu dhidi ya ubinaadam nchini Libya.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/KNA /dpa
Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman