Mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika kufanyika wiki ijayo
18 Januari 2018Masuala hayo ni pamoja na Mageuzi na fedha. Wachambuzi wanatarajia majadiliano makali katika mkutano huo.
Iwapo maneno ndio msingi wa kila kitu, basi Afrika imara na yenye amani ni kipaumbele kikubwa kwa viongozi wengi wa Afrika. Lakini suala kuu kwa viongozi hao watakaohudhuria mkutano wa kilele wa 30 wa Umoja wa Afrika watatafuta mikakati juu ya vipi hali hiyo inaweza kupatikana. mkutano huo muhimu utaanza rasmi katika makao makuu wa Umoja huo katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa Januari 22.
Viongozi wa mataifa 55 wanachama wa Umoja wa Afrika watakutana kujadili njia za kuimarisha hali ya maisha barani Afrika na kuufanyia mageuzi Umoja wa Afrika ili kwamba uwe katika nafasi nzuri ya kufanikisha malengo muhimu. Viongozi wa Afrika tayari mwaka jana walikubaliana kuufanyia mageuzi Umoja huo.
Chombo hicho cha bara la Afrika kinakabiliwa na matatizo ya fedha na kukosa uwezo wa kugharamia operesheni zake za kulinda amani. Bado ni tegemezi kwa misaada ya kifedha kutoka nje. Mwaka 2015 , asilimia 75 ya bajeti yake ya uendeshaji ilitoka kwa wafadhili wa kimataifa, kama Marekani na Umoja wa Ulaya.
Wakosoaji
Wakosoaji pia wanadai kwamba Umoja huo umekuwa ukiburuza miguu mno kuchukua hatua dhidi ya hatari za kiusalama.
Rais wa Rwanda Paul Kagame anaongoza juhudi za mageuzi. Julai mwaka jana , alichaguliwa kuchukua nafasi ya rais wa Guinea Alpha Conde kuwa mwenyekiti wa AU. Rwanda imechukua wadhifa wa uenyekiti wa Umoja wa Afrika mwanzoni mwa mwaka 2018. Mapendekezo ya mabadiliko tayari yako mezani. Kwa mujibu wa Kagame , nguzo kuu ya mageuzi ya AU yanapaswa kuwa ni uwezo wa kujigharamia.
"Ni hatari kwa Afrika kutegemea kwa kiasi kikubwa vyanzo vya fedha ambavyo kuna uwezekano mkubwa wa kukauka haraka kuliko hapo baadaye, hususan wakati tuna uwezo wa kulipia mipango ambayo ina faida kwetu," aliandika Kagame katika taarifa iliyochapishwa katika gazeti la New Times mjini Rwanda wiki hii.
"Ni muhimu kuendeleza misingi na dhamira ambayo inahamasisha kuleta mageuzi, wakati huo huo kuonesha uwezo wa kubadilika katika masuala fulani ambako mataifa wanachama wanataka," Kagame aliongeza.
Yann Bedzigui , mtafiti katika taasisi ya mitaala ya kiusalama mjini Addis Ababa pia anafikiri kwamba Umoja wa Afrika unapaswa kuendeleza msukumo huo wa hivi sasa. "Tunapaswa kuendelea ili kuweza kuleta athari ya muda mrefu," alikiambia kituo cha matangazo cha DW. Bedzigui anahisi kwamba AU tayari imekwisha piga hatua kubwa ikilinganishwa na mtangulizi wake, Umoja wa nchi za Afrika OAU.
Utekelezaji wa hatua za mageuzi
"Kiasi ya theluthi mbili ya fedha zinatoka kwa wafadhili, hivi sasa wanapaswa wao wenyewe kufanyakazi ili kuweza kuongeza michango ya mataifa ya Afrika.
Hatua fulani zimekwisha pigwa katika nyanja hii. Mataifa wanachama yamekubaliana kuhusiana na pendekezo la kugharamia Umoja wa Afrika kwa michango ya asilimia 0.2 ya kodi zitokanazo na bidhaa zitakazoingizwa katika mataifa hayo kuanzia Julai mwaka jana.
Mataifa 20 wanachama yametia saini kwa ajili ya mfumo huu na nchi 14 zimo njiani kuutekeleza.
Kwa mujibu wa Alex Vines , mkurugenzi wa mpango wa Afrika katika taasisi ya kukusanya mawazo ya Chatham House, kuna tatazo la kuelewana, kwa sababu baadhi ya jumuiya za kanda, kama ECOWAS tayari zinatekeleza kodi ya kuingiza bidhaa kutoka nje ili kugharamia shughuli zao. Hii huenda ikawa na maana mataifa ya Afrika magharibi hayatakuwa na hamasa ya kupandisha kodi hiyo.
Vines anahisi kwamba kuna mapendekezo mazuri kwa mageuzi ya AU mezani, lakini masuali juu ya utekelezaji bado yanaendelea kuwako.
Mwandishi: Schwikowski, Martin / ZR / Sekione Kitojo
Mhariri: Daniel Gakuba