1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa siku tatu kuhusu afya ya uzazi waanza mjini London

ELIZABETH KEMUNTO30 Agosti 2004

Mkutano unafanyika mjini London na lengo la kutazama njia mpya zitakazotumiwa kutimiza malengo ya mkutano uliofanyika Cairo miaka kumi iliyopita, kufikia mwaka wa 2015.

https://p.dw.com/p/CEHf

Zaidi ya wajumbe mia saba wanakutana leo mjini London Uingereza ili kuyaangalia upya makubalino yaliyoafikiwa katika mkutano kuhusu idadi na maendeleo, miaka kumi iliyopita. Mashirika yasiyo ya kiserikali tayari yamefanya mkutano na kutayarisha njia za kukabiliana na makubaliano yaliyoafikiwa mjini Cairo Misri miaka kumi iliyopita.

Mkutano huo unaojulikana kama countdown 2015 unafanyika kuadhimisha nusu ya miaka iliyowekwa kwa ajili ya kutimiza malengo yaliyowekwa katika mkutano wa Cairo. Kwa sababu serikali hazikutani kabla ya mkutano mwingine kama ule uliofanyika mjini Cairo mashirika yasiyo ya kiserikali yameamua kukutana ili kuangalia nini kimetekelezwa na nini bado kinahitaji kufanywa. Afya ya uzazi inajumuisha mambo kama vile kupanga uzazi, kuzuia ukimwi na magonjwa mengine ya zinaa na njia salama za kujifungua.

Kufikia sasa fedha ambazo zimetolewa na wafadhili kwa ajili ya kutekeleza malengo hayo, ni nusu ya kile kiwango kinacho takikana.

Kama maafikiano hayo ya tangu miaka kumi yatakuwa na matokeo yoyote, hali ya mambo katika baadhi ya nchi ni lazima irekebishwe. Tuchukue mfano wa Sierra leone. Sierra Leone ni nchi ndogo inayopakana na bahari ya Atlantik lakini inajulikana sana duniani kwa kuwa na visa vingi zaidi vya akina mama kufa wakati wa kujifungua. Yvonne Harding ambaye anafanya kazi na shirika la Marie Stopes International, anasema kuwa idadi ya akina mama wanaokufa nchini Sierra Leone ni 2,100 kwa kila wanawake laki moja wanaojifungua. Shirika hilo linatoa huduma za afya ya uzazi katika nchi thelathini na nne duniani.

Harding aliongeza kuwa vifo vya watoto wachanga ni mia moja na sabini kwa kila watoto elfu moja wanaozaliwa. Miaka anayotarajiwa mtu kuishi ni thelathini na nne.

Lakini Harding anasema kuwa hali haikuwa mbaya hivyo hapo awali. Kati ya mwaka wa 1990 na 1991 idadi ya wanawake waliofariki wakijifungua ilikuwa ni robo ya idadi ya wanaokufa sasa. Mojawapo ya sababu ya idadi hii kupanda ni mzozo wa wenyewe kwa wenyewe kati ya waasi na serikali, ambao ulisababisha vifo vya maelfu ya watu. Mamilioni wengine ambao ni zaidi ya thuluthi moja ya idadi ya watu nchini humo, waliachwa bila makao.

Nyenzo mbinu nchini humo zilivunjika kabisa afya ikiwemo. Huduma za afya zingali zinapambana kurudia hali ya zamani. Marie Stopes International imeweka vituo saba vya kutoa huduma za afya ya uzazi nchini humo.

Hata hivyo shirika hilo linakabiliwa na matatizo kwani bidhaa za kupanga uzazi kama vile mipira ya kondom, vidonge vya kumeza vya wanawake na madawa hayapatikani na hivyo kulazimu shirika hilo kuyatoa nchi za nje. Shirika hilo limetoa malalamiko kuwa haliruhusiwi kutekeleza utoaji mimba. Barani Afrika, ni Afrika Kusini na Cape Verde tu ambako utoaji wa mimba unakubaliwa kisheria.

Watu wanaohitaji huduma ni wengi kuliko uwezo wa shirika hilo kuwahudumia. Shirika hilo linahitaji kutoa huduma zote za afya ya uzazi, kutibu magonjwa ya zinaa na kutoa mafunzo au habari kwa watu. Bei ya madawa inahitaji kupunguzwa kwani watu wengi hawana pesa za kuyanunua na ili kufanya mambo haya yote fedha shirikahilo linahitaji pesa.

Ni jukumu la mashirika kama vile Marie Stopes International kuhakikisha kuwa kuna fedha za kutimiza malengo yaliyowekwa na serikali za nchi mbali mbali mjini Cairo. Hakuna haja ya malengo hayo kuwa makaratasini kama hayawezi kutimizwa.

Serikali za Afrika zimeweka sheria hapa na pale kuhusu afya ya uzazi lakini kwa kweli hakuna mabadiliko makuu katika sekta hiyo na hasa kuhusu vijana ambao ni asilimia arobaini na nne ya idadi ya watu barani Afrika. Mkutano wa London ni lazima uangalie zaidi mahitaji ya Afrika kwa sababu ndio inahitaji huduma za afya ya uzazi kuliko nchi nyengine.