Mkutano wa Trump na Kim kuendelea kama ulivyopangwa
2 Juni 2018Rais wa Marekani Donald Trump amesema mkutano wa kilele kati ya Korea Kaskazini na Marekani utafanyika Juni 12 kama ilivyopangwa awali.
Tangazo la Trump limejiri baada ya mjumbe wa ngazi ya juu wa Korea Kaskazini Kim Yong Chol kumkabidhi Trump barua kutoka kwa kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un.
Kufuatia mazungumzo na mjumbe huyo Kim Yong Chol katika ikulu ya White House, Trump aliwaambia waandishi wa habari kuwa kuwa katika mkutano huo wa kilele na kihistoria, watajadili suala la kumaliza kabisa silaha za nyuklia katika rasi ya Korea na kumaliza rasmi vita vya miongo mingi vya Korea.
Trump: Kumalizwa kwa mpango wa nyuklia katika rasi ya Korea ni mchakato
Marekani inataka Kim kukubali kile maafisa wa Marekani wanasema ni hatua zinazothibitika na zisizoweza kurejelewa za kumaliza mipango ya silaha za nyuklia za Korea Kaskazini na makombora ya masafa marefu yanayoweza kurushwa kutoka bara moja hadi jingine.
Kim amesema yuko tayari kumaliza kabisa silaha za nyuklia katika rasi ya Korea, lakini anatarajiwa kuwa na matakwa ya kiusalama, kama kumalizwa rasmi kwa mzozo kati ya nchi yake na Korea Kusini pamoja na Marekani.
Wataalamu wengi wanatashwishi ikiwa mkutano kati ya viongozi hao wawili utapelekea kupatikana kwa suluhisho la haraka. Rais Trump amesema hatua zote ni mchakato mrefu na mgumu.
Waziri wa ulinzi wa Marekani Jim Mattis amesema kuwa suala la wanajeshi wa Marekani kuwa nchini Korea Kusini halitajadiliwa katika mkutano huo wa Trump na Kim.
Mwandishi: John Juma/AFPE
Mhariri: