Mkutano wa Umoja wa Afrika wavunjika
1 Julai 2011Viongozi wa Afrika waliunga mkono mpango wao wa upatanishi wa mgogoro wa Libya katika siku ya kwanza kabisa ya mkutano huo hapo jana, ambao unafanyika katika mji mkuu wa Guinea ya Ikweta, Malabo.
Mkutano huo wa vuta n'kuvute pia umehudhuriwa na pande zote hasimu nchini Libya, yaani utawala wa Gaddafi na Waasi. Hata hivyo, maafisa wanasema ungendelea tena baadae.
Mpango huo wa upatanishi wa Umoja wa Afrika unajumuisha kusimamisha mapigano, misaada ya kiutu, kipindi cha mpito, mabadiliko kulekea demekrasia na uchaguzi, lakini ufafanuzi na nafasi ya Gaddafi katika masuala hayo haijawa wazi.
Mwakilishi wa Baraza la Mpito la Waasi, Mansour Safy Al-Nasr, aliwaambia waandishi wa habari kwa upande wao bado unashinikiza kwamba Gaddafi aliyekuwa madarakani kwa zaidi ya miaka 40 aondoke.
Mwakilishi hiyo wa waasi aliongeza kwa kusema kwamba Gaddafi mwenyewe anafikiri mgogoro huo utamalizika kisiasa au kijeshi, basi wao wako tayari kwa namna yeyote ile. Na kwamba Waasi hawatosalimu amri kwa wakati huu.
Al-Nasr alisema kama operesheni za kijeshi zikisonga mbele na kuzunguka mji wa Tripoli, Gaddafi atakubali kuondoka madarakani. Hivi sasa amejitenga. na kudai yupo katika handaki lake, hana maisha, hawezi kwenda kokote.
Nae mwenyekiti wa Baraza la Waasi, Mahmud Jibrir, ambae kwa hivi sasa yupo mjini Vienna, alisema anangoja msimamo wa wazi kutoka kwa Umoja wa Afrika kwama wanamuunga mkono au wanamlaani Gaddafi.
Jibril aligusia kutolewa kwa waranti wa kukamatwa Gaddafi, akisema unaashiria kwamba mauwaji yamefanyika, kwa hivyo Umoja wa Afrika unapaswa kuwa wazi katika suala hilo.
Umoja wa Afrika, kwa upande wao, umesema waranti huo uliotolewa na mahakama ya kimataifa ya uhalifu unafanya mambo yawe magumu katika kufikia suluhisho la mgogoro wa Libya.
Pia umesema hali imekuwa tete na hasa Ufaransa ilipoanza kutoa silaha kwa waasi, ukiachilia mbali malalamiko ya mwanzoni kuhusu mashambulizi ya ndege za Umoja wa Kujihami.
Wakati huo huo, mapambano yanaendelea nchini Libya. Taarifa za hivi punde zinaeleza kwamba waasi nchini humo wamejiondoa katika eneo la karibu na mji wa Bir al-Ghanam, huko kusini mwa Tripoli, baada ya kuvurumishiwa makombora ya mareketi na wanajeshi watiifu kwa Gaddafi.
Mwandishi: Sudi Mnette/AFP/RTR
Mhariri: Miraji Othman