Mkutano wa viongozi wakuu wa AU kuanza
29 Januari 2014Kwa mujibu wa waziri wa mambo ya nje wa Ethiopia Tedros Adhanom mkutano huo wa kilele wa viongozi wakuu wa nchi na serikali za Afrika´unaofanyika leo (30.01.2014) utazungumzia zaidi kuhusu mgogoro unaoendelea katika Jamhuri ya Afrika ya Kati pamoja na Sudan Kusini huku pia suala tete juu ya dhima ya bara hilo kwenye mahakama ya Kimataifa ya inayoshughulikia uhalifu wa kivita ICC likitarajiwa kugusiwa.
Kimsingi mkutano huo wa kila mwaka ulipangiwa kulijadili suala zima ya kilimo na usalama wa chakula nchi hizo wanachama lakini zinategemewa kuliweka kando au kulipa uzito mdogo suala hilo na badala yake kujikita zaidi katika kuishughulikia migogoro inayowakabili wanachama wenzao.
Katika Suala la Sudan itakumbukwa kwamba hapo jana rais wa Kenya Uhuru Kenyatta alitangaza mafanikio kiasi yaliyopatikana katika kujaribu kuumaliza mvutano unaoshuhudiwa ambayo yanajumuisha kuachiwa huru kwa wanasiasa wakuu saba kutoka upande wa waasi unaoongozwa na makamu wa rais wa zamani Riek Machar,jambo ambalo limekuwa siku zote mzizi wa fitna katika mgogoro huo wa Sudan Kusini.Rais Kenyatta alisema Umoja wa Afrika na Igad wamejitolea katika kuisaka amani ya kudumu katika taifa hilo changa barani Afrika,
Sudan Kusini, Afrika ya Kati kujadiliwa
Mazungumzo ya amani yakiongozwa na jumuiya ya ushirikiano wa kiserikali katika nchi za mashariki mwa Afrika IGAD ilifikia uamuzi wa kuyafuta mazungumzo hayo wiki iliyopita baada ya kupatikana mwafaka wa kusitisha mapigano huku wasuluhishi wakitowa mwito wa kutaka Umoja wa Afrika ubebe jukumu kubwa katika mchakato huo wa kutafuta amani nchini Sudan Kusini.
Kwa mujibu wa mhadhiri kutokachuo cha SOAS mjini London Uingereza Phil Clark mojawapo ya masuala ambayo Umoja wa Afrika utalazimika kuyafafanuwa kwa uwazi katika mkutano huu itakuwa ni kuhusu dhima itakayoibeba katika mgogoro huu.Baadhi ya wachambuzi wanahisi shinikizo huenda likahitajika kutokea upande mmoja wa Umoja wa Afrika wenye mamlaka .
Kwa upande mwingine janga la Jamhuri ya Afrika ya Kati ambako kuna kikosi kizito cha wanajeshi 5,200 wa Umoja wa Afrika waliopelekwa kupambana bega kwa bega na kikosi cha wanajeshi 1,600 wa Ufaransa ni mada itakayochukuwa nafasi nyingine ya mkutano huo .
Nchi hiyo ilitumbukia vitani miezi 10 iliyopita baada ya waasi kuiangusha serikali na kuchochea ghasia za kidini zilizosababisha mauaji makubwa. Hata hivyo kwa mujibu wa wachambuzi wa masuala ya kisiasa Umoja wa Afrika unaweza kukosolewa kutokana na jinsi ilivyojitokeza kushughulikia migogoro na hasa Suidan Kusini na Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Agenda 2023
Umoja wa Afrika kwa mujibu wa wadadisi hauoneshi uongozi thabiti katika kuitatuwa mizozo hii na hayo ndiyo mambo yatakayoangaziwa zaidi.Fauka ya hayo Umoja huo wa Afrika unategemewa pia kuzungumzia kile kinachoitwa Agenda 2023 ,mpango wa malengo ya Umoja huo baada ya miaka 50 tangu kuasisiwa kwake.
Halikadhalika hapo jana mkuu wa halmashauri ya Umoja huo wa Afrika Nkosazana Dlamini Zuma aliwaondolea wasiwasi wale wanaodhani kwamba anaweza kuutupa mkono wadhifa wake huo na kukimbilia kukiwakilisha chama tawala nchini mwake ANC bungeni.Zuma amezipuuzilia mbali ripoti hizo akisema hana nia ya kukatiza wadhifa wake huo katika Umoja wa Afrika na yeye daima amekuwa mwanachama wa ANC nchini mwake na ataendelea kubakia kuwa hivyo.
Mwandishi:Saumu Mwasimba
Mhariri:Mohammed AbdulRahman