Mkuu wa ofisi ya rais wa DRC, Vital Kamerhe atiwa mbaroni.
9 Aprili 2020Vital Kamerhe anashukiwa kwa kosa ubadhirifu wa fedha za serikali ila wafuasi wa UNC wanamatumaini na sheria ya Kongo, licha ya kuwa wamekerwa kuona kiongozi kama huyo ametupwa jela badala ya kuwekwa chini ya ulinzi katika kizuizi cha nyumbani. Vital Kamerhe amelala katika gereza kuu la Makala la mjini Kinshasa kwa siku yake ya kwanza usiku wa kuamkia leo hii, ambako alipelekwa na polisi baada ya kusikilizwa na korti ya Matete kwa muda wa masaa sita Jumatano.
Kiongozi wa ofisi ya rais Felix Tshisekedi ambaye pia ni kiongozi wa chama cha Muungano kwa Taifa la Kongo, UNC, anatuhumiwa kwa ubadhirifu wa fedha za serikali zilizokuwa zimetengwa kwa maendeleo ya nchi, yaani mpango wa siku 100 wa rais.
Vital Kamerhe si wa kwanza kutiwa mbaroni.
Tuhuma za Kamerhe zinawagusa viongozi wengine.
Mahakama ya Kinshasa imewahi kuwasikiliza na kuwaweka mbaroni baadhi ya waheshimiwa wengine waliohusika na mpango huo, ila wengi miongoni mwa wakongomani walionyesha umuhimu wa kumsikikiza pia kiongozi wa ofisi ya serikali kwani ni yeye alikuwa na mamlaka yote kuhusu fedha zinahusika na mpango huo na mipango na mikataba yote ilipitia kwake.Na korti kuu ya Matete ya Kinshasa ilifuatilia jambo hilo na kumualika Vital Kamerhe kama shahidi, na baadaye, Kamerhe kawekwa chini ya ulinzi wa polisi na kuchukuliwa moja kwa moja hadi jela kuu la Makala.
Chama cha UNC chalaani kukamatwa kwa Kamerhe.
Chama cha UNC kilisema kinategemea sheria ya Kongo ichukue mkondo wake ila kinachokera ni hiyo hatua ya kumweka kizuizini badala ya kumuweka chini ya ulinzi nyumbani kwake. Chama UNC cha Vital Kamerhe na kile cha Muungano kwa Demokrasia na Maendeleo ya Jamii, UDPS, chama chake rais Felix Tshisekedi ndivyo vilivyo madarakani, baada ya kushirikiana na kuunda muungano CACH kwa lengo la kuongoza pamoja.
Wanaharakati wanaolenga mabadiliko yaani LUCHA wameridhishwa na kuwekwa kwake mbaroni mkuu wa ofisi ya rais, ili kuruhusu uchunguzi bora katika tuhuma za rushwa na pia ubadhirifu wa fedha hapa nchini. Tangu siku chache zilizopita, wafuasi wa chama cha UDPS na wale wa UNC walikuwa hawashirikiani tena vyema. Baadhi ya wanainchi wana hofu kuwekwa gerezani Vital Kamerhe kunaweza kukasababishi vurugo hapa nchini.
Mwandishi: Jean Noel Ba-Mweze, DW, Kinshasa.