Mkuu wa Wagner asema anasaka mamluki wapya Afrika
22 Agosti 2023Kwenye video iliyosambaa siku ya Jumatatu (Agosti 21) kwenye mitandao, kiongozi huyo wa kundi la Wagner anasikika akisema yuko huko aliko kufanya kazi kukiwa na joto la nyuzi 50 kwenda juu.
"Kundi la Wagner linaendesha kampeni ya mwamko na shughuli za kusaka. Tunaifanya Uruis kuwa na nguvu zaidi kuliko mabara yote. Na tunaifanya Afrika kuwa huru zaidi. Sisi tunapigania haki na furaha ya watu wa Afrika." Anasema kwenye mkanda huo.
Soma zaidi: Sudan: Kundi la Wagner na vita vya kuwania madaraka na dhahabu
Yevgeny Prigozhin atangaza kuwasajili wapiganaji wapya
Kwenye kipande hicho cha video ya sekunde 40, Prigozhin anaonekana akiwa amevalia magwanda ya jeshi na bunduki mkononi katika ardhi kavu ya jangwa na, kwa mujibu wa maelezo yake, ndani ya nchi moja barani Afrika.
"Tunawaogofya ISIS, Al-Qaida na magenge mengine. Tunakodi mashujaa wa kweli na tunaendelea kutimiza majukumu yaliyowekwa na tuliyoahidi kuyatekeleza." Anasikika akisema.
Bado hakujawa na taarifa huru inayothibitisha video hiyo wala undani wa mahala na tarehe hasa ilipochukuliwa, lakini inafahamika kuwa mamluki hao wa Kirusi, waliojizolea umaarufu kwa ukatili wao, wako kwenye mataifa kadhaa barani Afrika.
Wagner sehemu ya kampeni ya kijeshi ya Urusi
Kwa miezi kadhaa pia, wapiganaji wa Wagner wamekuwa wakipambana bega kwa bega na jeshi la Urusi baada ya uvamizi wa nchi hiyo dhidi ya Ukraine ulioanza Februari 2022.
Mwishoni mwa Juni, Prigozhin aliwaongoza wapiganaji wake kuandamana kuelekea Moscow kwa kile alichosema ni kufadhaishwa na ugoigoi wa uongozi wa jeshi la Urusi, lakini walizuiwa masaa machache baadaye kupitia majadiliano kati yake na serikali chini ya upatanishi wa Belarus.
Soma zaidi: Touadera: Je, ni mtu wa amani ama "Rais Wagner"?
Blinken: Kundi la Wagner linatumia mapinduzi ya Niger kwa manufaa yake
Ilisemekana kuwa Kremlin ilimuahidi Prigozhin kinga ya kutoshitakiwa kwa sharti la kuhamishia shughuli zake nchini Belarus.
Hata hivyo, mkuu huyo wa kundi la Wagner alionekana tena nchini Urusi kwenye vikao vya mkutano wa kilele kati ya Urusi na Afrika mjini St. Petersburg mwishoni mwa mwezi Julai.
Katika siku za hivi karibuni, kumekuwa na wasiwasi kwamba Niger inaweza sasa kuegemea zaidi upande wa Moscow baada ya mapinduzi ya kijeshi kumuondowa kiongozi anayependelewa na mataifa ya Magharibi, Mohamed Bazoum, na ambayo yalipongezwa na Prigozhin.
Mkuu huyo wa Wagner aliyaita mapinduzi hayo kuwa sehemu ya vita vya taifa hilo la magharibi mwa Afrika dhidi ya wakoloni.
Vyanzo: AFP, dpa