MOGADISHU:Watu 5 wauawa na bei za vyakula kupanda wakati wa Ramadhan
18 Septemba 2007Watu 5 wameuawa katika ghasia mpya nchini Somalia pale wapiganaji kutoka koo ndogo zinazohasimiana za Habel-Gedir walipambana katika bandari ya Merka iliyo umbali wa kilomita 100 kusini mwa mji mkuu na kusababisha vifo vya watu 3.Kiongozi wa koo hiyo Hajj Hussein Adan alithibitisha vifo hivyo na kuongeza kuwa ghasia hizo zilisababishwa na mauaji ya naibu kamanda wa polisi Muhamud Salat Sanjaebil anayetoka kwenye koo moja ndogo husika.
Wengine wawili waliuawa katika mapigano ya usiku kucha kati ya Somaliland na Puntland maeneo ya kaskazini mwa Somalia yanayozozania eneo la mpakani.Ghasia hizo zilitokea katika eneo la Sool lililo kaskazini magharibi mwa Mogadishu.Mapigano hayo yalihusisha majeshi ya serikali kutoka eneo la Somaliland lililojitenga na wapiganaji wanaounga mkono serikali ya eneo jirani la Puntland.
Wakati huohuo Bei za vyakula nchini Somalia zinaripotiwa kuongezeka katika mwezi wa Ramadhan jambo linalotatiza raia wengi ambao ni Waislamu wanaokabiliwa na ghasia za kila siku.Vyakula vikuu nchini humo kama mchele,pasta na mafuta ya kupikia vimeongezeka bei maradufu jambo linalosababishwa na usalama duni vilevile msimu wa monsoon unaotatiza usafiri wa meli za chakula.